Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali kushadidi kwa machafuko na mapigano nchini Sudan Kusini, ambako watu wapatao milioni 10, wakiwa ni zaidi ya theluthi mbili ya idadi ya watu wote nchini humo, wanahitaji msaada wa kibinadamu wa kuokoa maisha na wanaendelea kuathirika zaidi na mgogoro huo.

Taarifa iliyotolewa na Guterres kupitia Naibu msemaji wa UN Farhan Haq imesisitiza kwa kusema: “Katibu Mkuu anazitaka pande zote kusitisha mara moja na kwa dhati operesheni zote za kijeshi, kupunguza mvutano kupitia mazungumzo, kuheshimu sheria za kimataifa, kuwalinda raia, na kuhakikisha upatikanaji salama na endelevu wa misaada ya kibinadamu pamoja na usalama wa wafanyakazi wa misaada na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na mali zao,” imesisitiza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, upuuzaji wa waziwazi shughuli za tiba na misaada ya kibinadamu haukubaliki na lazima ukome mara moja na kwamba kazi hizo zinapasa kuwezeshwa na kuheshimiwa.

Mapigano, mashambulizi na uporaji wa vituo vya misaada ya kibinadamu na vya afya pamoja na vikwazo vya usafiri na hali ya kutokuwepo kwa usalama katika njia muhimu za usambazaji vinaathiri kwa kiasi kikubwa operesheni za huduma za kibinadamu na kusababisha kusitishwa huduma muhimu, hali inayowaweka raia, wakiwemo wafanyakazi wa misaada, katika hatari kubwa.

Tangu mwishoni mwa Desemba, karibu vituo 11 vya huduma za afya vimeshambuliwa katika Jimbo la Jonglei, jambo lililosababisha kuvurugika kwa huduma za kuokoa maisha. Mashambulizi hayo pia yamehusisha kutekwa kwa magari 12, likiwemo gari la wagonjwa.

Katika wiki moja iliyopita pekee, matukio kote nchini Sudan Kusini yamejumuisha mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya msafara wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), shambulio la anga dhidi ya hospitali inayoendeshwa na shirika la Madaktari Wasio na Mikapa, (Médecins Sans Frontières), pamoja na kuchomwa moto ofisi ya shirika la watoto la Save the Children na kuharibiwa kituo chake cha afya pia.

Zaidi ya watu 370,000 wameripotiwa kuyahama makazi yao kutokana na mapigano kote nchini humo mwaka huu pekee, wakiwemo zaidi ya watu 280,000 katika Jimbo la Jonglei, wakati mripuko wa maradhi ya kipindupindu pia ukiendelea kuongezeka kwa kasi…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *