Chanzo cha picha, Getty Images
Afrika Kusini imetangaza mipango ya kuwaondoa wanajeshi wake kutoka kwenye vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku ikieleza kuwa hatua hiyo ni ya muhimu ili kuunganisha na kupanga upya rasilimali za vikosi vyake vya ulinzi.
Tamko la Ikulu lilionesha kuwa Rais Cyril Ramaphosa alimjulisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kuhusu uamuzi huo mwezi Januari mwaka huu.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, “Afrika Kusini itafanya kazi kwa pamoja na Umoja wa Mataifa ili kuweka ratiba na taratibu nyingine za kutoa wanajeshi, ambazo zitamalizika kabla ya mwisho wa mwaka wa 2026.’”
Wanajeshi 700 wa Afrika Kusini wamepelekwa kusaidia vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini DRC na wamekuwepo nchini humo kwa kipindi cha miaka 27.
Pia, Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi kumi zinazochangia idadi kubwa ya wanajeshi katika vikosi vya MONUSCO, kwa lengo la kudumisha amani nchini humo.
Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vina jumla ya wanajeshi na polisi 11,000 waliotumwa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kama sehemu ya juhudi za kudumisha amani nchini humo, baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuongeza mwaka mmoja kwa vikosi hivyo kuwepo nchini humo Desemba 2025.
MONUSCO imekuwa ikifanya kazi kuwalinda wananchi dhidi ya makundi mbalimbali ya waasi yanayofanya shughuli zake Mashariki mwa DRC, ambapo hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la mapigano yaliyogubikwa ukatili mkali kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali.
Hatua hiyo imeibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa kudorora kwa usalama nchini DRC, hasa katika eneo la mashariki ambapo vurugu zimeongezeka. Serikali ya DRC imehoji ufanisi wa MONUSCO, na kuondoka kwa wanajeshi hao kunaweza kusababisha kutokuwepo kwa serikali maalum.
Hata hivyo, Afrika Kusini pia imedokeza kuwa itaendelea kudumisha uhusiano wa karibu na kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa (UN), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), na Umoja wa Afrika (AU) ili kuleta amani nchini DRC.