
Duru za habari zimearifu kuwa ulinzi mkali umeimarishwa baada ya milio mikali ya risasi kusikika mapema leo karibu na gereza kuu katika mji mkuu wa Guinea, Conakry.
Bado haijafahamika nani amehusika na ufyatuaji risasi huo uliosikika leo huko Guinea Conakry.
Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo la ufyatuaji risasi ameeleza kuwa malori kadhaa ya jeshi yalionekana yakiwa yamewabeba askari usalama wenye silaha wakielekea karibu na wilaya ya kati ya Kaloum katika mji mkuu Conakry. Ikulu ya Rais ipo pia eneo hilo.
Askari usalama awali walizuia njia zinazoelekea katika gereza kuu huko Conakry ingawa baadaye njia hizo zilifunguliwa.
Takriban magari matatu ya kivita ya kikosi maalumu cha usalama yalionekana pia mbele ya gereza hilo na magari matatu ya kubebea wagonjwa yalishuhudiwa yakitoka katika gereza hilo kuu.
Gereza kuu la Guinea si geni kwa matukio ya vurugu. Mwaka 2023, watu tisa waliuawa kufuatia hujuma ya kuvunjwa gereza hilo kuu ambapo makomando kadhaa waliokuwa na silaha walifanikiwa kwa muda mfupi kumuachia huru kiongozi wa zamani wa kijeshi wa Guinea, Moussa Dadis Camara, na watu tisa walipoteza maisha.
Didas Camara na maafisa watatu wa zamani wa utawala wake ambao walikuwa wamefungwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji mwaka 2009, waliondolewa katika gereza hilo na muda mfupi baadaye walikamatwa na kurejeshwa gerezani.