Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth), kundi la mataifa 56 linaloongozwa na Mfalme Charles wa Uingereza, amesema anatarajia nchi wanachama wa jumuiya hiyo zitapiga hatua ya kuanza mazungumzo kuhusu fidia ya biashara ya utumwa iliyovuka Bahari ya Atlantiki.
Bi Shieley Botchwey aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Ghana mbaye ameunga mkono hadharani suala la kudai fidia kutoka kwa Uingereza, amesema anaunga mkono nchi wanachama wa jumuiya katika jitihada za kutafuta suluhisho la suala hilo.
“Uelewa wangu ni kwamba kuna harakati katika suala la kuamua namna ya kusonga mbele, na kuainisha aina tofauti za fidia,” amesema Shirley Botchwey.
Ameongeza kuwa majadiliano yatakuwa ya pande nyingi na yanaweza kuhusisha makundi ya kikanda kama Jumuiya ya Karibiani na Umoja wa Afrika.
Jumuiya ya Madola ambayo imetokana na dola la kikoloni la Uingereza, ni mojawapo ya taasisi kubwa zaidi za kimataifa, inayowakilisha karibu watu bilioni 2.7. Wanachama wake ni pamoja na Australia, India, mataifa 21 ya Afrika na nchi za Karibea kama vile Barbados na Jamaica.
Mfalme Charles wa Uingereza amesema anajutia sana suala la utumwa na ameunga mkono utafiti kuhusu uhusiano wa kihistoria wa dola la kifalme la Uingereza na biashara hiyo. Hata hivyo, Uingereza, kama yalivyyo mataifa mengi ya zamani ya kikoloni, inapinga wito wa kulipwa fidia ya kipindi cha utumwa.
Kuanzia karne ya 15 hadi 19, Waafrika wasiopungua milioni 12.5 walitekwa nyara na kuuzwa kama watumwa na wafanyabiashara wa Ulaya.

Uingereza ilihusikka katika kusafirisha takriban watu milioni 3.2, na nafasi hiyo iliifanya kuwa nchi ya pili ya Ulaya kuhusika pakubwa katika biashara ya utumwa baada ya Ureno, ambayo iliwafanya watu karibu milioni sita kuwa watumwa.
Mwaka jana Umoja wa Afrika uliliweka katika ajenda ya mkutano wake wa kila mwaka suala la kuzilipa fidia nchi za Kiafrika na kutaka kuchukuliwe msimamo wa pamoja katika uwanja huo.