
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ametoa tahadhari kuhusu azma ya utawala wa Israel ya kuishawishi Marekani iingie katika vita vingine dhidi ya Iran, wakati mazungumzo mapya ya nyuklia kati ya Tehran na Washington yakiwa yameanza.
Mwanadiplomasia huyo mkuu aliyasema hayo katika mahojiano na kituo cha Russia Today siku ya Jumanne, alipohojiwa kuhusu ziara inayotarajiwa ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika Ikulu ya White House, ambapo inasadikiwa atalenga kuvuruga mchakato wa kidiplomasia unaoendelea.
Araghchi amemtaja Netanyahu kuwa ni “mchochezi wa vita” asiye na mapenzi na amani wala diplomasia. “Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ameshambulia nchi saba katika eneo letu,” amesema waziri huyo, na kuongeza kuwa hata Qatar ambayo ni mshirika wa Marekani na Magharibi ilishambuliwa.
Kwa mujibu wa Araghchi, Netanyahu “hana suluhisho jingine akilini mwake isipokuwa vita,” na kwa muda mrefu amekuwa akijaribu “kuivuta Marekani iingie vitani na Iran.”
Afisa huyo ameashiria uchokozi wa hivi karibuni wa utawala wa Israel, ambapo Washington iliungana na Tel Aviv katikati ya vita vilivyoanzishwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu mwezi Juni. Alilitaja tukio hilo kuwa “janga” kwa Israel na Marekani, akiashiria hatua za kali za kulipiza kisasi zilizochukuliwa na Iran ambazo, ziliilazimisha Tel Aviv kuomba usitishaji mapigano kupitia Washington.
Inaripotiwa kuwa katika ziara hiyo ijayo, waziri mkuu wa Israel atajaribu kumshawishi rais wa Marekani ajumuisha suala la mpango wa makombora wa Iran katika ajenda ya mazungumzo. Hata hivyo, Tehran imekataa kwa kauli moja wazo hilo, ikisisitiza kuwa uwezo wake wa makombora ni sehemu isiyotenganishwa ya nguvu zake za kujihami na hivyo ni haki yake ya kikatiba na ya kimsingi kama dola huru.
Kuhusu mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, ambayo duru yake ya karibuni ilifanyika Muscat, mji mkuu wa Oman, Ijumaa iliyopita, Araghchi amesema wajumbe wa Marekani, wakiwemo mkwe wa Rais Trump, Jared Kushner, pamoja na mjumbe wa kikanda wa Washington, Steve Witkoff, “wanajaribu kuepusha vita na kutafuta suluhu ya kidiplomasia.”
Hata hivyo, amekumbusha tena kuwa Netanyahu “hafurahishwi na ukweli kwamba mazungumzo yanaendelea vizuri.”