
Balozi wa Marekani katika shirika la kijeshi la NATO Matthew Whitaker amewafananisha na watoto wanachama wa kambi ya Ulaya katika shirika hilo, ambao amesema ni lazima hatimaye waache kuwa chini ya malezi na matunzo ya mzazi wao wakatafute kazi.
Siku ya Jumatatu wiki hii, waandaaji wa Mkutano wa Usalama wa Munich (MSC), ambao umepangwa kufanyika kuanzia Februari 13 hadi 15, walieleza katika ripoti yao ya kila mwaka kwamba: “kwa miongo kadhaa, Ulaya imestawi chini ya mwavuli wa usalama wa Marekani ambao umeiruhusu itoe kipaumbele kwa utangamano na ustawi kuliko kujizatiti katika nguvu kali za kijeshi. Zama hizo zimekwisha.”
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa ripoti hiyo, Whitaker alisema: “sikubaliani hata kidogo na kila nilichokisikia.” Washington “haikusudii kuibomoa NATO,” alieleza balozi wa Marekani katika shirika hilo la kijeshi na kuongeza kuwa, lakini kitu pekee inachotaka ni kuona nchi za Ulaya zinabeba jukumu zaidi kwa ajili ya ulinzi wao.
“Watoto wako wanapokuwa wadogo, wanakutegemea. Lakini hatimaye unawatarajia wapate kazi. Na kwa hiyo kwangu mimi, hapo ndipo tulipo. Tungali tunawapenda. Ninyi mngali ni washirika,” alisisitiza balozi huyo wa Marekani kuiambia hadhira kwa kutumia lugha iliyotafsiriwa na baadhi kuwa ni ya kuzidunisha nchi za Ulaya.
Katika mwaka wake wa kwanza madarakani, serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump imetangaza mara kadhaa kwamba itapunguza kutekeleza ahadi zake kwa nchi za Ulaya, huku ikijikita kwenye “kulinda ardhi ya Marekani na kuzuia hujuma za China”…/