
Rais wa Marekani Donald Trump ameeleza baada ya kukutana na waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba mkutano huo ulikuwa “mzuri sana” na akasema: “nimesisitiza kwamba mazungumzo na Iran inapasa yaendelee.”
Baada ya mazungumzo yake na Netanyahu, ambayo kwa mujibu wa vyombo vya habari yalichukua takribani muda wa masaa matatu, Trump alisema mkutano huo wa faragha ulikuwa mzuri sana na kwamba uhusiano imara uliopo kati ya pande hizo mbili unaendelea.
Trump alifafanua: “hakukuwa na maamuzi ya wazi yaliyofikiwa isipokuwa nilisisitiza kwamba mazungumzo na Iran inapasa yaendelee ili kuona kama makubaliano yanaweza kufikiwa.”
Kufuatia madai yasiyo ya kimantiki ya Washington kwa Tehran, Rais wa Marekani aliendelea kutoa kauli zenye mgongano kwa kusema: “ikiwa makubaliano yatafikiwa, nilimtaka waziri mkuu ajue kwamba hiki ndicho kipaumbele chetu. Ikiwa hayatafikiwa, tutaona nini yatakuwa matokeo yake”.
Duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani ilifanyika Ijumaa ya Februari 6, 2026, huko Muscat, kwa usimamizi wa Ufalme wa Oman kupitia waziri wake wa mambo ya nje Bad bin Hamad Al Busaidi.
Pande hizo ziliyaelezea mazungumzo hayo kwamba yalikuwa “mazuri” na kuonyesha nia ya kuyaendeleza.
Katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa Jumanne usiku na tovuti ya habari ya Axios, Trump alisema anatarajia duru ya pili ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran itafanyika wiki ijayo…/