
Upigaji kura unaendelea nchini Bangladesh katika uchaguzi muhimu unaoonekana kama mtihani muhimu wa kurejea kwa demokrasia nchini humo baada ya vuguvugu la umma lililoongozwa na wanafunzi kumng’oa madarakani kiongozi wa muda mrefu Sheikh Hasina mnamo Agosti 2024.
Uchaguzi huo wa leo ni ushindani wa moja kwa moja kati ya Chama cha Kitaifa cha Bangladesh (BNP) na muungano wa vyama 11 unaoongozwa na Jamaat-e-Islami, ikiwa ni pamoja na Chama cha Kitaifa cha Wananchi (NCP), kilichoundwa na wanaharakati vijana waliotoa mchango mkubwa katika kumwondoa Hasina madarakani.
Tarique Rahman wa BNP na Shafiqur Rahman wa Jamaat wamepiga kura zao katika mji mkuu Dhaka huku tume ya uchaguzi ikipongeza idadi kubwa ya watu waliojitokeza. Karibu watu milioni 127 wametimiza masharti ya kupiga kura katika nchi hiyo yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 175 .
Rushwa, mfumuko wa bei, ajira na maendeleo ya kiuchumi ndio masuala makuu yanayoamua uchaguzi katika taifa hilo la nane lenye watu wengi zaidi duniani.
Mbali na uchaguzi wa bunge, Wabangladesh wanashiriki katika kura ya maoni kuhusu Mkataba wa Kitaifa wa 2025 – hati iliyoandikwa na serikali ya mpito inayoongozwa na Muhammad Yunus, ikiweka msingi wa utawala wa siku zijazo…/