Klabu ya Nottingham Forest imemtimua kazi kocha wake, Sean Dyche kufuatia matokeo ya Suluhu dhidi ya Wolves yaliyoiacha Klabu hiyo ikizidi kusuasua katika vita ya kujinusuru kushuka daraja.
Dyche, mwenye umri wa miaka 54, anakuwa kocha wa tatu kufutwa kazi na mmiliki wa klabu hiyo, Evangelos Marinakis, ndani ya msimu huu baada ya Nuno Espirito Santo na Ange Postecoglou pia kuondolewa awali.
Kocha huyo aliteuliwa Oktoba mwaka jana wakati timu ilipokuwa sehemu salama, lakini anaondoka akiwa ameiacha Forest ikiwa katika hatari ikipambana kujinusuru kushuka daraja.
Katika michezo 22 ya Ligi Kuu aliyoiongoza, Dyche amekusanya pointi 18 pekee. Hata hivyo, ameisaidia timu kufuzu hatua ya mchujo ya Europa League ambapo watakutana na Fenerbahce katika michezo miwili, mechi ya kwanza ikitarajiwa kupigwa jijini Istanbul wiki ijayo.
Aliyekuwa kocha wa Nottingham Forest, Sean Dyche, ambaye amefukuzwa kazi baada ya mwendelezo wa matokeo mabaya Klabuni hapo. Picha na Mtandao
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa usiku wa kuamkia leo, klabu hiyo imesema:
“Tunapenda kumshukuru Sean na benchi lake la ufundi kwa jitihada zao wakiwa hapa klabuni na tunawatakia kila la heri huko waendako. Hatutatoa maoni zaidi kwa sasa.”
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Jarida la Daily Mail, zinaeleza kuwa aliyekuwa kocha wa Wolves, Vitor Pereira, ni miongoni mwa wanaopewa nafasi ya kuchukua mikoba hiyo.
Pereira aliwahi kutimuliwa na Wolves Novemba mwaka jana kufuatia mwanzo mbaya wa msimu, lakini amesifiwa kwa kuirejesha timu hiyo katika mstari mzuri na kuinasua kwa kishindo baada ya kutua Desemba 2024.
Akizungumza kabla ya kutimuliwa kwake, Dyche ameonekana kukubaliana na hali halisi ya soka la kisasa, akisema mabadiliko ya makocha ni sehemu ya mchezo.
Baadhi ya wachezaji wa Nottingham Forest wakiwashukuru mashabiki waliojitokeza kuwasapoti uwanjani baada ya mechi hiyo kumalizika. Picha na Mtandao
“Katika soka la sasa, kama mmiliki ataamua kufanya mabadiliko, hilo ni jukumu lake. Hivyo ndivyo hali ilivyo,” amesema Dyche.
Ameongeza: “Sina tatizo na mmiliki. Amekuwa mwadilifu kwangu tangu mwanzo hadi mwisho, nami nimekuwa mkweli kwake kila hatua. Mahitaji yameongezeka sana katika miaka miwili iliyopita, matarajio yanapanda haraka. Lakini hakuna njia rahisi katika Ligi Kuu. Hatuko kwenye mwendo mbaya sana, lakini tupo sehemu isiyofaa kwenye msimamo na matokeo yanaeleza ukweli.”
Forest sasa wanatarajiwa kuanza harakati za kumteua kocha mpya haraka iwezekanavyo huku vita ya kubaki Ligi Kuu ikiendelea kupamba moto.