Wadau wa soka wamesema kuwa njia ya majadiliano ndio sahihi kwa sasa yanayoweza kumaliza migongano inayoendelea ndani ya Simba baina ya upande wa wanachama na mwekezaji.

Ushauri huo umetolewa siku mbili baada ya mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji kuibuka na kuhoji mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo ulipofikia huku Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Murtaza Mangungu akijibu mapigo kwa kurudisha mpira kwa bilionea huyo akisema ndiye anapaswa kutoa majibu ya alichokihoji.

“Transformation mmefikia wapi?,” alihoji Mohammed Dewji akichangia taarifa iliyotumwa na Simba mtandaoni ikinukuu kauli ya mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu kuhusu usajili wa Wanachama.

Hata hivyo jana, Mangungu alisema japo hajaona swali hilo lililoulizwa na Dewji, mwekezaji huyo ndio anatakiwa aulizwe kuhusu hatima ya mchakato huo.

“Binafsi sijaona na nasikia tu lakini nyie mnapaswa kumuuliza yeye kwa nini ametumia njia hiyo na kwa nini ameuliza hivyo. Mimi sina ninachoweza kujibu, sina jibu. Kwa sasa mchakato wa ‘Transformation’ unaendelea na upo katika vyombo vya serikali,”alisema Mangungu.

Wakizungumza na Mwananchi hili kwa nyakati tofauti jana, wadau wa soka wamesema kuwa kuna ishara za wazi kuwa upande wa mwekezaji na wanachama mambo hayako sawa hivyo wanapaswa kutatua hilo kwa njia za majadiliano.

“Maoni yangu siku zote ni kwamba wale wanaosababisha tatizo ndio wanapaswa kutatua tatizo. Nadhani ni jambo linalohitaji busara kulitatua kwa vile Simba ni taasisi kubwa ambayo inagusa hisia za watu wengi na taasisi nyingi mfano wadhamini,” alisema Mjumbe wa zamani wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tulliy.

Makamu Mwenyekiti wa zamani wa Simba Godfrey Nyange ‘Kaburu’ ameshauri viongozi wa Simba kukaa pamoja na kuanza mpya mchakato mzima.

“Kwa maoni yangu naamini Dewji ameshaona anachokitaka hawezi kukipata. Kuna makosa yalishafanyika nyuma kama vile Baraza la Wadhamini kusaini makubaliano na mwekezaji na pia kamati ya tenda kutangaza mshindi wakati wakijua sheria haiko hivyo.

“Nadhani ni vyema kwa sasa katiba ikishapita, viongozi wakae na serikali kwa maana ya Baraza la Michezo, Msajili na pia wanachama wa Simba, ili watengeneze ramani ya kupita. Thamani ya Klabu ijulikane na tenda itangazwe upya. Ni lazima wakubaliane ili mambo yaende vizuri,” alisema Kaburu.

Wakili Mwandamizi wa masuala ya Michezo, Aloyce Kombe amesema kuwa mchakato unapaswa uwe shirikishi.

“Kinachoamriwa na Mkutano Mkuu kinapaswa kuwa cha mwisho na hakitakiwi kuwepo na mtu wa kukipinga. Kama kuna migongano au kuna jambo wanaona haliko sawa au wanahitaji utafsiri wa katiba na sheria, wanapaswa kurudi kwa msajili na baraza ili kupata ufafanuzi,” alisema Komba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *