Dar es Salaam. Msanii wa Hip-hop nchini Rashid Abdallah ‘Chid Benz’, amesema marehemu mama yake, Hawa Idd alimuonesha ushirikiano kwenye sanaa tangu siku ya kwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 12, 2026, Chid amesema mama yake alikuwa akihudhuria kwenye shoo zake. Kumuandikia nyimbo na kumsaidia kwenye masuala ya kifedha kwa ajili ya kuendesha sanaa yake.
“Mama yangu ameanza kunisapoti kuanzia siku ya kwanza. Ndio maana alikuwa anakuja kwenye shoo, mama yangu alikuwa anaweza kuandikia muziki na mashairi.
“Alinichagulia ngoma zangu hit ikiwemo ‘Dar es Salaam Stand Up’, na hela za kuendeshea muziki wangu,” amesema Chid.
‘Dar es Salaam Stand Up’ ni wimbo uliotoka mwaka 2011. Umekuwa ukiendelea kuwarusha mashabiki wa msanii huyo kila akiimba.
Aidha msanii huyo ameeleza ratiba ya mazishi ya mama yake, kuwa utapumzishwa Chanika, Dar es Salaam leo Februari 12, 2026, saa saba mchana. Ikumbukwe mama yake Chid alifariki dunia jana Februari 11, 2026 nyumbani kwake.