Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Muhi al-Din Salem Ahmed amekariri wito wake kwa Umoja wa Afrika, akiitaka AU kufuta hatua yake ya kuisimamishia uanachama nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika umoja huo.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa jana Alkhamisi, Salem amesema mzozo nchini Sudan umefikia tamati.

“Vita sio lengo letu na tutaendelea kutafuta amani,” mwanadiplomasia huyo mkuu amesema katika matamshi yake yaliyonukuliwa na vyombo vya habari vya Sudan, akisisitiza kwamba serikali ya Khartoum inaendelea na juhudi zake za kufikia amani ya kudumu nchini humo.

Aidha ameshutumu baadhi ya maajibani kwa kuchochea mzozo nchini Sudan, bila kuwataja majina, na Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) kwa kutumia rasilimali za dhahabu kinyume cha sheria katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake.

Waziri Salem ameashiria jukumu la Sudan katika kulinda bara la Afrika kutokana na kile alichokiita vitisho mbalimbali, hasa kwa kutumia silaha za kigeni na kueleza kuwa, “Kubatilisha hatua ya kusimamishiwa uanachama Sudan AU kutaifaidi Afrika.” 

Mapigano ya sasa Sudan yalianza Aprili 2023 wakati waasi wa RSF walipoanzisha vita dhidi ya serikali kuu ya Sudan kwa lengo la kunyakua madaraka. Makumi ya maelefu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni 12 kulazimika kuwa wakimbizi ndani ya nje ya Sudan.

Khartoum inaituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa inawaunga mkono waasi hao wa RSF wanaoendelea kufanya mashambulizi na jinai nyinginezo kila uchao nchini Sudan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *