Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, uwepo wa meli za Iran katika bahari na maji ya kimataifa ni mseto wa nguvu za kijeshi na diplomasia ya baharini.
Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefafanua vipengele mbalimbali vya safari za hivi karibuni za misafara ya meli za kivita za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika maji ya nje ya eneo hili. Amesema uwepo wa manowari za Iran katika bahari za mbali na maji ya kimataifa hakumaanishi kutumwa meli za kijeshi tu, bali ni dhihirisho la mchanganyiko wa nguvu za kijeshi na diplomasia ya baharini, uwezo wa kisayansi na kiteknolojia, maadili ya kibinadamu na kutumwa ujumbe wa utamaduni wa Kiislamu kwa jamii ya kimataifa.
Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: ‘Utayarifu na uwezo mkubwa katika kutekeleza kwa usahihi majukumu hususan katika maji ya kimataifa na ulinzi wa njia muhimu za mawasiliano ya baharini umedhihirishwa wazi na hivyo kuweka wazi uwezo mkubwa wa kikosi hiki katika kulinda maslahi ya taifa.’
Akiashiria nafasi ya mwongozo wa kistratijia wa Amiri Jeshi Mkuu, Admireli Shahram Irani amesisitiza kwamba: ‘Sehemu kubwa ya maendeleo na mafanikio hayo inatokana na mwongozo wenye busara wa Kiongozi Muadhamu, ambaye amefungua njia kwa ajili ya kufikiwa ubora na ustawi wa Jeshi la Wanamaji.’
Kwa mtazamo wa kistratijia, misheni za muda mrefu za vikosi vya wanamaji vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika bahari za mbali na maji ya kimataifa zinaimarisha nguvu za kuzuia hujuma za Iran. Uwepo hai katika misheni za utoaji misaada ya kibinadamu, mapambano dhidi ya uharamia na ushirikiano wa kimataifa unaiwasilisha Iran sio tu kama jeshi la kawaida bali kama mhusika muhimu anayeleta utulivu.

Kuwepo kwa manowari za Iran katika maji ya kimatifa kunapaswa kuchukuliwa kama ishara ya kina ya kistratijia na ukomavu wa pande kadhaa wa jeshi la wanamaji wa Iran. Mbali na kudhamini usalama na nguvu, uwepo huu ni wenzo madhubuti katika kudhihirisha uwezo wa kielimu, kidiplomasia na kiutamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa kimataifa. Katika hali ambayo Ghuba ya Uajemi na hasa Lango Bahari la Hormuz inachukuliwa kuwa moja ya maeneo nyeti zaidi ya nishati na biashara ya kimataifa, kuimarika nguvu za kijeshi za Iran katika maji ya kieneo na kimataifa, sio hatua ya kimaonyesho tu, bali pia ni stratijia ya kiulinzi.
Uwepo huu una ujumbe wa wazi kwa madola yanayotumia mabavu duniani kwamba Iran inaweza kudhamini maslahi yake ya kitaifa na usalama wa njia zake za mawasiliano popote katika maji ya kimataifa bila kutegemea nchi nyingine. Hili ni dhihirisho la nguvu ya uzuiaji madhubuti na kujiamini kiulinzi, hasa kwa kutilia maanani kukiri kwa viongozi wa nchi za Magharibi kuhusiana na ukuaji wa kasi wa uwezo wa jeshi la majini la Iran.
Uchoraji, ujenzi na uhifadhi wa manowari na nyambizi ndani ya nchi unaonyesha kudhibitiwa mzunguko kamili wa maarifa asilia ya uhandisi wa hali ya juu nchini. Uwezo huu kielimu umelifanya Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufikia utoshelevu kamili wa kiutendaji katika ngazi ya kistratijia na kutekeleza majukumu nyeti katika maji ya kimataifa bila kutegemea miundombinu ya kigeni.
Mbali na nyanja za kijeshi na kiufundi, uwepo wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unabeba ujumbe wa kiutamaduni na wa kibinadamu. Ujumbe huu umejikita katika mtazamo wa Kiislamu na kiustaarabu wa nchi, ambao unachukulia nguvu si kama chombo cha ubeberu na ukandamizaji, bali kama njia ya kutetea haki, usalama wa pamoja na utukufu wa mwanadamu.
Tabia na mienendo ya wafanyakazi wa jeshi la majini katika misheni za kimataifa imejengeka kwenye misingi ya maadili kama vile utu, kuhifadhi mazingira ya baharini, ushirikiano wa amani na mataifa mengine na kuzingatia misingi ya maadili ya usafiri wa baharini. Mtazamo huu umegeuza nguvu ya kijeshi ya Iran kuwa nguvu ya kimaadili, jambo linaloonyesha sura tofauti ya uwepo wa kijeshi baharini.
Uwepo wa manowari za Iran katika maji ya kimataifa unaonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kuweka uwiano wa kistratijia kati ya nguvu ya zana za kijeshi na nguvu laini, yaani masuala ya kiutamaduni, kidiplomasia na kimaadili, na hivyo kuimarisha nafasi yake kama mmoja wa wahusika wanaowajibika na wenye nguvu katika medani ya bahari duniani.