Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (droni) za wanamgambo wa kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) yameuwa raia wawili na kujeruhi wanne katika jimbo la Kordofan Kusini. Haya yamebainishwa jana Mtandao wa Madaktari wa Sudan.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeripoti kuwa shambulio la droni la RSF lililenga eneo la al Kurqal linalounganisha miji ya Dilling na kadugli. Baadhi ya majeruhi wana hali mbaya kwa mujibu wa taarifa ya awali ya madaktari waliofika katika eneo la tukio. 

Mtandao huo umesemam kuwa shambulio la ndege zisizo na rubani za wanamgambo wa RSF lililenga katika eneo la raia wengi  kufuatia kuzorota kwa hali ya kibinadamu na kiafya na kuitaja hujuma hiyo kuwa uhalifu kamili na kuwatuhumu wanamgambo wa RSF kwa kutojali maisha ya raia wa Sudan.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema kuwa uongozi wa RSF unabeba dhima ya mashambulizi hayo huko Kordofan Kusini. Umetaja mashambulizi hayo kuwa sehemu ya mchakato mpana wa ukiukwaji wa mara kwa mara dhidi ya raia katika maeneo mengi ya Sudan, hali inayozidisha mateso kwa raia na kudhoofisha juhudi zozote za kulinda maisha yao na kuwadhaminia utulivu wa kiwango fulani.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeitolea wito jamii ya kimataifa, Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu kuchukua hatua kali kusitisha vitendo vyote vya ukiukaji wa haki za binadamu na kuzidisha mashinikizo ili kuwalinda raia. 

Hadi sasa hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na wanamgambo wa RSF kuhusu mashambulizi ya jana huko Kordofan Kusini. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *