#HABARI: Shahidi wa tano wa Jamhuri katika kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ametoa ushahidi wake Mahakamani akieleza jinsi alivyoshawishiwa na hotuba za kiongozi huyo.

Shahidi huyo wa siri anayetambulika kama “P 6,” ambaye ni dereva bodaboda mwenye umri wa miaka 24 kutoka Songea, alitoa maelezo hayo akiwa ndani ya chumba maalumu ili kulinda utambulisho wake mbele ya majaji na upande wa mashtaka.

Shahidi huyo alieleza kuwa alianza kukifuatilia chama cha CHADEMA mnamo Oktoba 2024 kwa kuhudhuria mikutano ya hadhara na kufuatilia viongozi mbalimbali, akiwemo Tundu Lissu na viongozi wa vijana mkoani Ruvuma.

Ilipofika Januari 2025, alivutiwa na kutaka kuwa mwanachama rasmi wa chama hicho, ambapo alielekezwa na kiongozi wa wilaya kuhusu taratibu za kupata kadi ya chama, ingawa mchakato huo ulichelewa kutokana na changamoto za kiufundi.

Ilielezwa mahakamani kuwa mnamo Aprili 4, 2025, akiwa kazini, shahidi huyo alitumia simu yake kusikiliza hotuba ya Lissu kupitia mtandao wa YouTube. Katika hotuba hiyo, alimshuhudia Lissu akihamasisha ajenda ya kuwa bila mabadiliko hakuna uchaguzi, akitumia maneno kama “tunakwenda kukinukisha” na “tunakwenda kuvuruga uchaguzi,” huku akiwataka watu kuungana naye katika agenda hiyo ya kuzuia mchakato wa uchaguzi.

P 6 alihitimisha ushahidi wake kwa kusema kuwa hotuba hiyo ilimfanya aamini kuwa hakutakuwa na kugombea udiwani, ubunge, wala urais kama mabadiliko hayatafanyika.

Alikiri kumfahamu Lissu kama mwanasiasa mkongwe na maarufu, na kusisitiza kuwa maneno hayo yalimuingia na kumshawishi kuwa miongoni mwa watu waliokuwa tayari kuunga mkono harakati za kuzuia uchaguzi mkuu kama mabadiliko ya kisheria hayatafikiwa.

Powered by #MCHEZOSUPA

JINSI YA KUSHIRIKI MCHEZO SUPA:

Tuma 1000 kupitia Airtel Money, Tigo Pesa, M – Pesa, Halopesa, kwenda namba ya kampuni 222223 kumbukumbu namba ni 777 au weka neno ITV.

#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania
#Follow @itvtz @radioonetanzania
@capitaldigitaltanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *