Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito mkali wa kuhakikisha haki na mageuzi yanatekelezwa na kuimarishwa ushirikiano wa kimataifa, huku akiutaja Umoja wa Afrika AU, kama “kinara wa ushirikiano wa kimataifa katika dunia iliyogawanyika”.

Guterres ametoa wito huo leo alipohutubia Mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa. 

Aidha, ametoa shukrani zake za dhati kwa msaada “thabiti na wa maamuzi” aliopata kwa umoja huo katika kipindi chote cha uongozi wake.

“Katika dunia iliyojaa mgawanyiko na kutoaminiana, Umoja wa Afrika ni kinara wa ushirikiano wa kimataifa,” amesema Katibu Mkuu wa UN na kusisitiza kwamba: “kila mara maamuzi kuhusu Afrika na dunia yanapojadiliwa, Afrika lazima iwe mezani.”

Guterres amesema, kukosekana kwa uwakilishi wa kudumu wa Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa “ni jambo lisilokubalika,” akisisitiza haja ya mageuzi ya haraka ya mfumo wa utawala wa kimataifa.

“Huu ni mwaka 2026 sio 1946,” amesisitiza, akimaanisha kuwa taasisi za kimataifa lazima ziakisi uhalisia wa sasa wa kisiasa na kiuchumi.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kuimarishwa Mfuko wa Hasara na Uharibifu unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, na kuhakikisha minyororo ya thamani ya madini muhimu inakuwa ya haki na endelevu.

Amesema, “hakuna tena uporaji. Hakuna tena unyonyaji. Watu wa Afrika lazima wanufaike na rasilimali za Afrika.”

Halikadhalika, Guterres amepongeza mchango wa Afrika katika kuunda Mkataba wa Zama Zijazo na kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na umoja huo, ikiwemo kupitishwa kwa Azimio namba 2719 la Baraza la Usalama, lililoweka njia ya ufadhili wa uhakika kwa operesheni za kulinda amani zinazoongozwa na AU…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *