Makundi ya Wapalestina na nchi kadhaa za eneo zimetoa mjibizo kwa mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuvamia na kuyakalia kwa mabavu maeneo kadhaa ya ardhi za Ukingo wa Magharibi, zikisisitiza kwamba, huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, HAMAS imetoa taarifa ikilaani hatua ya hivi karibuni ya baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni ya kuyasajili maeneo kadhaa ya ardhi za Ukingo wa Magharibi kwa anuani ya “ardhi za serikali,” na kuuelezea uamuzi huo kuwa ni jaribio la kutwisha maamuzi ya kivamizi na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Mohamed Ahmed Alyammahi, Spika wa Bunge la Kiarabu, naye pia amelaani uamuzi huo wa baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni akisisitiza kwamba huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria na irada ya kimataifa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, imesisitiza kupitia taarifa yake kwamba, kuna udharura kwa jamii ya kimataifa kuungana ili kuushinikiza utawala ghasibu wa Israel usimamishe mara moja utekelezaji wa uamuzi huo na kuzuia matokeo yake hatari.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, nayo pia imetoa taarifa ikionya kwamba, hatua hiyo hatari inalenga kuimarisha udhibiti wa utawala wa Kizayuni katika maeneo unayoyakalia kwa mabavuu na kudhoofisha haki za kisheria za watu wa Palestina.
Baraza la mawaziri la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel limeidhinisha mpango ambao, kwa mara ya kwanza tangu vita vya mwaka 1967, unauruhusu utawala huo ghasibu kutangaza sehemu kubwa ya ardhi za Ukingo wa Magharibi kuwa eti ni “ardhi za serikali”.
Kwa mujibu wa vipengele vya vya mpango huo, ardhi zote za Ukingo wa Magharibi ambazo hazijawasilishwa kwa hati za umiliki wa binafsi zitasajiliwa kama ardhi za serikali.
Uamuzi huo unaokiuka waziwazi sheria za kimataifa, utahamishia sehemu kubwa ya ardhi za Ukingo wa Magharibi kwenye uvamizi na umiliki wa utawala wa kizayuni. Lakini pamoja na hayo, viongozi wa Kizayuni wanajaribu kuitetea hatua hiyo kuwa ni ya kisheria na kuficha sura yake halisi ya ughasibu na uvamizi. Kuhusiana na hilo, wametangaza kwamba, mchakato huu utafanyika polepole, kwa hadhari na baada ya kukamilisha uchunguzi wa kisheria.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa, mpango wa utawala wa Kizayuni wa kujimilikisha maeneo kadhaa ya ardhi za Ukingo wa Magharibi za Palestina unayoikalia kwa mabavu unatambuliwa kama “ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa” na hatua hiyo inapingana moja kwa moja na mfumo wa sheria za kimataifa. Sababu muhimu zaidi ya mpango huo wa baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni kulaaniwa kimataifa ni kuendana kwake na upanuzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa kizayuni.
Sheria za kimataifa zimepiga marufuku vikali kuwahamishia watu kwenye eneo linalokaliwa kwa mabavu (Kifungu cha 49 cha Mkataba wa Nne wa Geneva). Ardhi zinazosajiliwa kama “ardhi za serikali” mara nyingi hutumika kwa ajili ya upanuzi wa vitongoji vya utawala wa Kizayuni.
Hatua hiyo inadhoofisha haki za kisheria za watu wa Palestina za kujiamulia mustakabali wao na kunufaika na rasilimali zao za kitaifa. Maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama yanasisitiza kila mara kuhusu ulazima wa kulindwa ardhi yote pamoja na haki za watu wa Palestina.
Mchakato wa kusajili hati za mali binafsi chini ya mfumo wa kisheria unaosimamia maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu ni mgumu mno au takribani hautekelezeki kwa Wapalestina; na lengo kuu la hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni ni “kuzatiti udhibiti wake kwa maeneo unayoyakalia kwa mabavu na kudhoofisha haki za kisheria za watu wa Palestina.”

Mpango huo wa baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni si utaratibu wa kiidara tu, bali ni mpango wa kivamizi wenye malengo ya ubaguzi wa rangi na ya kujipanua, na unapingana kikamilifu na msimamo rasmi wa kimataifa kwamba ujenzi wa vitongoji na ubadilishaji muundo wa ardhi za maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ni ukiukaji wa wazi wa sheria.
Mijibizo mikali iliyotolewa na Hamas, wadau wa kikanda na serikali mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Bunge la Kiarabu, na Wizara za Mambo ya Nje za Qatar na Misri, yote hiyo inaonyesha kuwa, hatua iliyochukuliwa na baraza la mawaziri la utawala wa kizayuni itakuwa na matokeo makubwa hasi kwa matukio ya Palestina na eneo kwa ujumla. Mijibizo hiyo ni miito ya kutaka yatumike mashinikizo ili kusimamisha mwenendo huo mara moja na kuzuia “matokeo yake hatari”…/