Awamu ya kwanza ya mazoezi ya Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imefanyika katika visiwa vya Iran kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi.
Mazoezi ya Jeshi la Wanamaji la IRGC yalifanyika kwa mafanikio Jumatatu (Februari 16) kwa kupitia mbinu na kutumia silaha mpya.
Katika mazoezi hayo, vikosi vya radiamali ya haraka vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, vilivyoko kwenye visiwa vya Iran vya Ghuba ya Uajemi, vilifanya mazoezi ya mbinu mpya za kushambulia na kujilinda. Katika mazoezi hayo, vitengo vya makombora vilijaribu aina mpya zaidi za makombora, mbinu za mapigano ya makombora na operesheni za vita vya kielektroniki.
Vitengo vya ndege zisizo na rubani na vya chini ya ardhi vya Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia vimeharibu shabaha zilizoainishwa katika mazoezi hayo, kutokea kwenye visiwa vitatu vya Iran. Awamu kuu ya mazoezi hayo iliendelea jana Jumanne (Februari 17) katika Mlango-Bahari wa Hormuz kwa operesheni ya udhibiti makini wa mlango-bahari huo wa kimkakati.
Admirali Alireza Tangsiri, Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesisitiza kwamba ufuatiliaji wa kijasusi wa IRGC katika Mlango-Bahari wa Hormuz ni saa 24 kwa siku, na kusema: “Usimamizi huo kamili” unalenga kuhakikisha usalama wa usafirishaji kupitia njia ya kimkakati ya majini.”

Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la IRGC amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kuhakikisha usalama wa Mlango-Bahari wa Hormuz na kuzuia ukosefu wa usalama katika eneo hilo. Amesema: Ni muhimu kulindwa maslahi ya nchi zote zisizohasimiana katika usafirishaji wa kupita njia hii, na Jeshi la IRGC limedhamini usalama huo kupitia matumizi ya zana, mifumo na doria za kawaida.
Mazoezi ya majini ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika visiwa vya Iran vya Ghuba ya Uajemi na Mlango-Bahari wa Hormuz ni mojawapo ya matukio muhimu zaidi ya kijeshi katika eneo hilo; kwani maeneo hayo ni kiunganishi na njia muhimu zaidi ya usafirishaji wa nishati duniani. Mlango-Bahari wa Hormuz hupitisha mamilioni ya mapipa ya mafuta kuelekea kwenye masoko ya kimataifa kila siku, na tishio lolote au ukosefu wa usalama katika eneo hilo unaweza kuathiri moja kwa moja uchumi wa dunia. Mbali na upande wake wa kijeshi, zoezi la IRGC ni maonyesho ya nguvu na uwezo wa Iran katika kudhibiti na kuhakikisha usalama wa njia hiyo ya maji ya kimataifa. Kwani, operesheni za mazoezi ya mbinu mpya, utumiaji wa makombora makini, ndege zisizo na rubani na vitengo vya chini ya ardhi za Jeshi la Wanamaji la IRGC zinaonyesha ustawi wa teknolojia ya kijeshi na kutegemea uwezo wa ndani. Mazoezi hayo yameonyesha kwamba Iran iko tayari kulinda mipaka yake ya baharini na ina uwezo wa kufanya operesheni za mashambulizi zenye ufanisi.
Tangazo la IRGC la kudhibiti kikamilifu taarifa zote za kijasuusi na kiintelijensia katika ngazi zote (nchi kavu, anga, na chini ya maji), linatuma ujumbe wa wazi kwa nchi za kikanda na nje ya kanda hii kwamba, usalama wa Ghuba ya Uajemi na Mlango-Bahari wa Hormuz lazima ulindwe kwa ushirikiano wa nchi za kikanda, na kwamba vikosi vya majeshi ya kigeni kama vile Marekani na washirika wake haviwezi kuwa na nafasi yoyote katika suala hilo.

Vilevile, kwa kufanya mazoezi ya kijeshi wakati huu, sambamba na ongezeko la harakati za vikosi vya majeshi ya Marekani katika eneo hilo na vitisho vya maneno vya nchi za Magharibi, Jeshi la Wanamaji la IRGC linatangaza kwamba Iran iko tayari kujibu ipasavyo jaribio lolote la kuvuruga amani katika eneo hilo. Kwa maneno mengine ni kuwa, mazoezi hayo ni ujumbe wa tahadhari kwamba kitendo chochote cha uchochezi kitajibiwa haraka na ipasavyo.
Mazoezi hayo pia yametuma ujumbe wa wazi kwa mataifa ya kikanda na kimataifa kwamba Iran inadhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi, lakini haikubali vitisho au uwepo wa vikosi vya majeshi ya kigeni. Pia inaonyesha kwamba vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran viko katika kiwango cha juu zaidi cha utayari wa kujilinda na kushambulia, na uvamizi wowote dhidi ya maslahi ya kitaifa ya Iran utakabiliwa na jibu la haraka.