
Vatican haitashiriki katika mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa iitwayo “Bodi ya Amani”. Hayo yameelezwa na afisa mkuu wa kidiplomasia wa Vatican Kardinali Pietro Parolin, huku akisisitiza kwamba juhudi za kushughulikia hali za mgogoro inapasa zisimamiwe na Umoja wa Mataifa.
Kardinali Parolin amebainisha kuwa, Vatican hakitashiriki katika bodi hiyo ya Trump kwa sababu ya hali maalumu iliyonayo.
Ametoa mfano kwa kusema: “hofu moja ni kwamba katika ngazi ya kimataifa inapasa juu ya wote uwepo Umoja wa Mataifa unaosimamia hali hizi za mgogoro. Hii ni moja ya nukta ambayo tumeisisitiza.”
Papa Leo, ambaye ni kiongozi mkuu wa kwanza wa Kanisa Katoliki raia wa Marekani na mkosoaji wa baadhi ya sera za Trump, alialikwa kujiunga na bodi hiyo mwezi Januari.
Chini ya mpango wa Trump wa Ghaza, ambao ulipelekea kufikiwa makubaliano tete ya kusitishwa vita mnamo mwezi Oktoba, bodi hiyo ilikusudiwa kusimamia uendeshaji wa muda wa Ghaza. Lakini muda kadhaa baadaye Trump alitangaza kwamba bodi hiyo, na yeye mwenyewe akiwa mwenyekiti wake, itapanuliwa ili kushughulikia migogoro ya kimataifa. Bodi hiyo iitwayo ya amani, itafanya mkutano wake wa kwanza huko Washington kesho Alkhamisi kujadili ujenzi mpya wa Ghaza.
Wakati huo huo, Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum ametangaza kwamba nchi yake haitashiriki kama mwanachama kamili katika bodi iliyoundwa na rais wa Marekani kutokana na kukosekana ndani yake uwakilishi wa Palestina.
“Kwa kuzingatia kwamba tunaitambua Palestina kama taifa, ni muhimu kwamba mataifa yote mawili, Israel na Palestina, yashiriki. Haijapangwa kuwa hivyo,” ameeleza rais huyo wa Mexico katika mkutano na waandishi wa habari.
Sheinbaum amebainisha kuwa, nchi yake itamtuma balozi wa Mexico katika Umoja wa Mataifa ashiriki kama mtazamaji.
“Walitualika kuhudhuria kama watazamaji; yaani kama hatutakuwa washiriki, basi tuhudhurie kama watazamaji. Na tumeamua kwa pamoja na waziri wa mambo ya nje, kwamba balozi wetu wa Umoja wa Mataifa ahudhurie kama mtazamaji” ameeleza kiongozi huyo.
Sheinbaum ametangaza uungaji mkono wake kwa Palestina, akitamka bayana kwamba mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya Ghaza na dhidi ya watu wa Palestina kuwa ni mauaji ya kimbari na kutoa wito wa kutekelezwa suluhisho la mataifa mawili…/