Marekani inatafakari juu ya kuiwekea vikwazo vikali Mahakama nzima ya Kimataifa ya Jinai (ICC) mapema wiki hii, hatua ambayo inaweza kuvuruga sana shughuli za mahakama hiyo katika kuchunguza uhalifu wa kivita uliofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel huko Ghaza.

Hapo awali, vikwazo vya Marekani viliwalenga waendesha mashtaka tu na majaji waliochaguliwa katika mahakama hiyo; hata hivyo, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kuijumuisha ICC yenyewe katika vikwazo hivyo kutamaanisha kushadidishwa mkakati wa kidiplomasia wa Marekani.

Vyanzo vingi vilivyozungumza kwa sharti la kutotajwa majina, vimeliambia shirika hilo la habari kwamba uamuzi kuhusu “vikwazo dhidi ya taasisi” hiyo unatarajiwa kuchukuliwa haraka.

Kwa kutarajia vikwazo vinavyoweza kuwekwa na Washington, maafisa wa ICC wameitisha mikutano ya dharura kutathmini madhara yanayoweza kutokea, huku mijadala ikifanyika kati ya wanadiplomasia wanaowakilisha nchi wanachama wa ICC.

Afisa mmoja wa Marekani amethibitisha kuwa vikwazo dhidi ya taasisi nzima ya ICC vinatafakariwa lakini hakutoa maelezo kuhusu wakati wa utekelezaji wake.

Ikiwa vikwazo hivyo vya Marekani vitatekelezwa dhidi ya ICC nzima, hatua hiyo inaweza kuhatarisha shughuli za kimsingi za mahakama hiyo, kuathiri mishahara, upatikanaji wa huduma za benki, na programu muhimu za ofisi.

ICC, ambayo makao yake makuu yako mjini The Hague, imewafungulia mashtaka viongozi wa ngazi za juu wa utawala wa kizayuni Israel, akiwemo waziri mkuu wake Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita, Yoav Gallant, kwa uhalifu uliofanywa wakati wa mauaji ya kimbari ya Ghaza.

Huko nyuma, Marekani ilishawahi kuwawekea vikwazo maafisa wa mahakama ya ICC kwa ufuatiliaji wao katika kesi hizo za Netanyahu na Gallant, pamoja na uchunguzi wa kabla yake kuhusu uhalifu uliofanywa nchini Afghanistan uliohusisha wanajeshi wa Marekani…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *