
SINGIDA Black Stars imerejea kwa kishindo katika Ligi Kuu Bara baada ya leo mchana kuifyatua Mtibwa Sugari kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma na kuchupa kutoka nafasi ya 13 hadi ya 10 ya msimamo wa ligi hiyo inayoelekea kukamilisha duru la kwanza kwa msimu huu.
Mechi hiyo ni ya kwanza kwa Singida tangu ilipong’olewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyoshiriki kwa mara ya kwanza na ilipata ushindi huo ulioifanya ifikishe pointi 15 kutokana na mechi tisa.
Hicho ni kipigo cha pili mfululizo nyumbani kwa Mtibwa kwani mechi iliyopita ilifumuliwa pia mabao 3-1 na Mashujaa inayonolewa na kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na jana iliruhusu kufungwa mabao kupitia kwa Mrundi Mossi Nduwumwe dakika ya 6 baada ya piga nikupige langoni mwa Mtibwa Sugar.
Dakika 11 baadae, Horso Muaku akifunga la pili akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Ibrahim Imoro aliyerejea Singida kutokea Mtibwa alikochezea kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu na bao la tatu liliwekwa kindiki cha pili kwa kichwa na nahodha Kennedy Juma dakika ya 54 akimalizika kona ya Andy Koffi.
Hata hivyo, jitihada za Mtibwa Sugar mwishoni mwa mechi hiyo, zilizaa matunda baada ya mshambuliaji wa kikosi hicho, Raizin Hafidh kufunga bao la kufutia machozi dakika ya 88, akimaliza krosi iliyopigwa na beki wa kulia, Datius Peter.
Ushindi huo kwa Singida unaifanya timu hiyo kusogea hadi nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kufikisha pointi 15, ambazo ni sawa na za Coastal Union iliyosogea nafasi ya 11 kutoka ile ya 10, kufuatia kucheza mechi tisa.
Kwa matokeo hayo, Mtibwa inaendelea kubakia katika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu na pointi 21, baada ya timu hiyo kushinda mechi tano, sare sita na kupoteza minne kati ya 15, iliyocheza, ikifunga mabao 13, huku ikiruhusu pia 14.