
BEKI wa kulia kinda wa timu ya vijana ya Yanga U-20, Isaack Mtengwa amejiunga na TRA United iliyopo Ligi Kuu kwa kwa mkopo wa miezi sita akitokea Wakiso Giants ya Ligi Kuu Uganda alikocheza msimu uliopita.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni mkakati wa kumpa dakika za kucheza na kuendelea kukua kisoka, hasa katika nafasi ya beki wa kulia inayohitaji uzoefu na utulivu mkubwa ndani ya uwanja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mtengwa amesema yupo TRA kwa mkopo wa miezi sita na malengo yake ni kuonyesha kiwango kizuri.
“Nashukuru Yanga kwa kuniamini na kunipa nafasi hii ya kwenda kucheza kwa mkopo. TRA ni timu nzuri yenye malengo, nimekuja kupambana na kuhakikisha ninatoa mchango wangu,” amesema Mtengwa na kuongeza;
“Kucheza Wakiso Giants kulinisaidia kujifunza vitu vingi, hasa kujiamini na kuwasiliana vizuri na mabeki wenzangu. Nimejifunza namna ya kukabiliana na presha ya mashindano.”
Katika msimu wake akiwa Uganda, Mtengwa alipata nafasi ya kucheza mara kadhaa kikosini hapo, ambapo katika ligi aliitumikia kwenye mechi tisa kwa dakika 450.
Nyota huyo ilikuwa mara ya kwanza kucheza Ligi Kuu Uganda, kwani hapo awali alizichezea timu za vijana za Simba na Yanga na baada ya kufanya vizuri akatolewa kwa mkopo ili kupata uzoefu kabla ya kurejea Jangwani na safari hii kutolewa kwa mkopo huo akiungana na nyota wengine.