
Mwana mtatanishi wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye ni mkuu wa majeshi ya nchi hiyo Muhoozi Kainerugaba ametoa matamshi yasiyo ya kawaida katika kumshambulia kiongozi wa wanamgambo wa Sudan wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF), Mohamed Hamdan Dagalo ambaye hivi karibuni alikutana na baba yake huko nchini Uganda.
“Hemedti ni mhalifu,” ameandika Muhoozi kwenye mtandao wa X Jumapili usiku, akimuashiria mkuu huyo wa RSF anayetambulika kwa lakabu hiyo. “Ana damu ya maelfu ya watu weusi mikononi mwake”, amesisitiza mkuu huyo wa majeshi ya Uganda.
Katika andiko lake hilo, Kainerubaga ameendelea kueleza: “RSF wanajihisi kama mashujaa kwa kuwaua watu weusi wasio na hatia. Vizuri sana. Naamini Hitler naye alijihisi kama shujaa pia kwa kuwachoma kwa gesi Wayahudi huko Auschwitz”.
Kainerugaba, ambaye licha ya kuwa na maazoea ya kutoa kauli za kichochezi na za utatanishi ndiye anatarajiwa sana kuchukua nafasi ya baba yake wakati Museveni atakapofariki, ameongezea katika ujumbe wake: “RSF italazimika kupigana na Afrika Nyeusi nzima kabla ya kushinda Sudan. Na hilo halitatokea KAMWE.”
Baada ya kuachana na utoaji shutuma kali dhidi ya kiongozi wa kundi la RSF la Sudan, Jenerali huyo wa Uganda amefichua kwamba anataka kutengeza sanamu la kaka wa waziri mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, Yoni, ambaye alikuwa kamanda wa jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel aliyefariki mwaka 1976 wakati wa uvamizi wa Entebbe wa kuwakomboa mateka wa kizayuni katika uwanja huo wa ndege wa Uganda.
“Kwa miaka minne iliyopita, mungu wangu Yesu Kristo amenijia ndotoni na kwenye maono. Ameniambia nitengeze sanamu la Yoni Netanyahu Entebbe. Na wala nisiiogope dunia. Yeye ana nguvu zaidi kuliko dunia”, ameendelea na utoaji wa kauli hizo tatanishi, mkuu huyo wa majeshi ya Uganda.
Wote wawili, Kainerugaba na baba yake, Museveni, wana uhusiano wa karibu na viongozi wa Israel, akiwemo Netanyahu.
Itakumbukwa kuwa, mnamo 2020, Museveni, pamoja na mkewe Janet, waliongoza mkutano muhimu kati ya Netanyahu na mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan, ambao ulionekana kama mwanzo wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Sudan na utawala wa kizayuni wa Israel…/