Njombe. Zaidi ya wafanyakazi 250 wa Kiwanda cha Chai cha Kibena Tea Ltd mkoani Njombe, wameanza mgomo wa kutokwenda kazini wakishinikiza kulipwa malimbikizo ya mishahara pamoja na michango yao ya hifadhi ya jamii.

Wafanyakazi hao wanadai licha ya kukatwa michango ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa zaidi ya miaka minane, fedha hizo hazijawasilishwa kwenye mfuko huo kama inavyotakiwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Februari 25, 2025, nje ya kiwanda hicho kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, wameema kwa kipindi chote hicho wamekuwa wakikatwa michango ya mafao kutoka katika mishahara yao, lakini walipofuatilia haki zao za mafao ya uzeeni waligundua kuwa haionekani katika kumbukumbu za NSSF.

Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, Isack Mhema amesema kuchelewa kulipwa malimbikizo ya mishahara kumesababisha maisha kuwa magumu na kushindwa kutimiza majukumu ya kifamilia.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Njombe kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Sigrada Mligo akiwa na viongozi wa kiwanda cha chai Kibena pamoja na wafanyakazi wa kiwanda hicho ambao wameitisha mgomo kushinikiza kulipwa malimbikizo ya mishahara pamoja na michango yao ya NSSF.

“Tunamuomba mwajiri wetu atulipe madai yetu kwa sababu tuna familia na maisha yamekuwa magumu sana,” amesema Mhema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani, Frida Kidenya amesema mwaka jana uongozi wa Kampuni ya DL Group, ulifanya kikao na wafanyakazi hao na kuwaahidi kuendelea kuwalipa madai yao kupitia mapato yatokanayo na biashara ya chai pamoja na uuzaji wa magogo ya misitu, huku ukiwataka waondoe hofu. Hata hivyo, mpaka sasa hawajalipwa.

Amesema mgomo huo ulianza Februari 5, 2026, ukiwa na lengo la kushinikiza uongozi wa kiwanda kujitokeza hadharani na kutoa ufafanuzi kuhusu sababu za kushindwa kuwalipa malimbikizo ya mishahara pamoja na kuwasilisha michango yao NSSF.

“Tumekuwa tukiahidiwa kwa muda mrefu na tulivumilia, lakini hatuwezi kuendelea kukaa bila majibu. Shida yetu kubwa ni mishahara yetu na michango yetu ya NSSF,” alisema Kidenya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Rasilimali Watu wa DL Group, Daniel Kairuki amekiri kuwepo kwa madai hayo na kusema kampuni inaendelea kutafuta utaratibu wa kushughulikia changamoto ya malimbikizo ya mishahara.

Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha chai Kibena, wakiwa na mabango yanayoshinikiza kulipwa madai yao ya malimbikizo ya mishahara mbele ya mbunge wa Njombe viti maalum Sigrada Mligo

Amesema mgomo wa wafanyakazi wa mashambani ulioanza Februari 5, mwaka huu umeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za uzalishaji wa zao la chai katika kiwanda hicho.

“Tunaendelea kufanya uchakataji wa madai ya wafanyakazi hawa, na wiki ijayo Mwenyekiti Mtendaji wa DL Group atakuwa na kikao na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF kwa ajili ya kufikia makubaliano,” amesema Kairuki.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Njombe kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Sigrada Mligo aliyefika kiwandani hapo, amewakutanisha wafanyakazi na viongozi wa kampuni hiyo ili kujadili namna ya kumaliza mgogoro huo.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili, amesema kuna haja ya uongozi wa kiwanda kushughulikia kwa haraka changamoto hizo na kutoa majibu ya madai ya wafanyakazi.

“Kwa mtazamo wangu, inaonekana kulikuwa na uzembe katika kulipa kwa wakati mishahara ya wafanyakazi, hali iliyosababisha malipo kulimbikizana,” amesema Mligo.

Amewataka wafanyakazi kuwa watulivu wakisubiri utekelezaji wa ahadi ya uongozi wa kiwanda, uliomuahidi mbele yake kuwa ndani ya wiki moja madai hayo yatakuwa yameshughulikiwa; vinginevyo, alisema ataungana nao katika hatua za kuitisha mgomo wa kufunga barabara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *