
Zanzibar. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yussuf Masauni amewataka Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuelimisha wananchi kuhusu misingi, faida na wajibu wao katika kulinda na kuutetea Muungano wa Tanzania.
Pia amewataka kupinga na kusahihisha upotoshaji wa taarifa kuhusu Muungano, hususan kupitia mikutano ya hadhara na mitandao ya kijamii, ili kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Masauni alitoa kauli hiyo leo Februari 27, 2026 wakati akifungua semina ya elimu ya Muungano kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ikiwa ni sehemu ya mpango unaoendelea wa kutoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya jamii.
Amesema Wawakilishi ni nguzo muhimu katika kulinda na kuimarisha Muungano kupitia majukumu yao ya kutunga sheria, kusimamia Serikali na kuelimisha wananchi katika majimbo yao.
“Wawakilishi mnabeba dhamana ya kihistoria ya kuhakikisha Muungano unaendelea kuwa chanzo cha amani, mshikamano wa pande mbili na maendeleo,” amesema Masauni.
Amebainisha kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wana nafasi kubwa ya kuifikisha elimu ya Muungano kwa wananchi kwa kuwa wako karibu zaidi na jamii na hukutana nao mara kwa mara.
“Wanawafikia wananchi wengi zaidi, hivyo wana wajibu wa kueneza elimu ya Muungano katika maeneo yao,” amesisitiza.
Masauni amesema mpango huo unawalenga kwa kiasi kikubwa vijana ili waweze kufahamu fursa zilizopo ndani ya Muungano na kuzitumia kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa fursa za Muungano ni nyingi, lakini changamoto iliyopo ni kutokuzitangaza na kuzifafanua ipasavyo kwa wananchi.
Kupitia semina hiyo, mada mbalimbali ziliwasilishwa zikiwemo chimbuko, misingi, umuhimu na upekee wa Muungano, kwa lengo la kuongeza uelewa na kujenga uzalendo wa dhati kwa nchi, pamoja na kuudumisha na kuuenzi Muungano kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.