Idara ya Polisi ya Kenya imetangaza mipango ya kuunda vikosi maalumu cha kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa usalama jijini Nairobi na katika miji mingine mikubwa huku nchi ikielekea katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Akizungumza katika makao makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Baharini (KMA) Mombasa wakati wa mkutano wa makamanda wakuu wa polisi kutoka kote nchini, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi ya Kenya, Eliud Lagat, amesema kuwa Idara hiyo imepokea maagizo madhubuti ya kukomesha wimbi linaloibuka la uhalifu.

“Hiyo ni sehemu ya mambo tunayojadili katika mkutano huu, amesema Eliud Lagat na kuongeza kuwa: Makamanda wa polisi wamepewa maagizo makali kushughulikia vitendo hivyo vya uhalifu katika maeneo yao ya uwajibikaji. Tunaunda vikosi maalumu kushughulikia hali hii na mtashuhudia msako ukiongezwa kwa kiwango cha juu zaidi,” amesema.

Mkutano huo wa siku tatu umewakutanisha pamoja makamanda wa polisi nchini Kenya, wakurugenzi na makamanda wa vitengo mbalimbali ili kupitia operesheni na mikakati ya kiusalama.

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi ya Kenya amesema sehemu ya majadiliano inalenga kusimamia usalama wakati nchi inajiandaa kwa kipindi cha kampeni na uchaguzi ujao.

Haya yanajiri huku visa vya uhalifu vikiongezeka katika maeneo ya mijini nchini Kenya, baadhi vikihusishwa na waendesha boda boda na magenge ya kihalifu.

Bw Lagat amesema vyombo vya usalama havitavumilia uhalifu unaojificha ndani ya sekta ya usafiri.

Ameonya kuwa waale wote wanaojihusisha na uhalifu hawana nafasi nchini na kwamba taasisi zote za serikali zitawachukulia hatua wahusika wa mashambulizi ya mapanga, biashara ya dawa za kulevya na pombe haramu kwa mujibu wa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *