SHINYANGA: WAJUMBE wa Chama Kikuu Cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) wamepitisha rasimu ya bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 2.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 huku ikijizatiti kuanza kukopesheka kwenye taasisi za kifedha.
Wajumbe hao wamepitisha bajeti hiyo leo Februari 28, baada ya Meneja wa SHIRECU, Alphonce Makasi kuwasomea taarifa na rasimu ya bajeti kwenye mkutano Mkuu wa 31 uliowakutanisha wajumbe 202 kati ya wajumbe 214 waliokuwa wakitakiwa kuhudhuria kwenye mkutano huo.

Makasi akisoma taarifa hiyo amesema wajumbe wakiridhia kupitishwa kwa bajeti zaidi ya Sh bilioni 2.8 na kukopa kwenye taasisi za kifedha wataweza kutimiza mipango ya kuendeleza biashara ya ununuzi wa mazao mchanganyiko,uanzishwaji na kufufua kiwanda kipya cha kukamua mafuta ya alizeti na kuendeleza duka la pembejeo.

“Taasisi za kifedha zilikataa kabisa kutukopesha kutokana na kuwepo kwa vikwazo vya deni kutoka benki ya Uwekezaji ya (TIB) lakini sasa tumeanza kuonyesha uaminifu wa kulipa na kupata ruhusa ya kuendelea kukopesheka kwenye taasisi za kifedha zozote nchini,”amesema Makasi.

Mwenyekiti wa Bodi ya SHIRECU, Naomi Chaba amesema kuna vyama vya ushirika (Amco’s) 107 na wanachama 7413 ambapo mpango ulioanza mwaka 2025 hadi Februari 2026 wamefanikiwa kununua mazao mchanganyiko kama choroko na dengu, kugawa kompyuta mpakato 50 nakutoa mafunzo,kukarabati shule ya sekondari Buluba na kusomesha wanafunzi 28 wa kidato cha tano kwa awamu kwa gharama ya Sh milioni 45.

Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Ibrahim Kakozi amesema taasisi za kifedha sasa zikae sawa kuwakopesha SHIRECU huku akiwataka wajumbe waeleze yale ambayo wanataka yatekelezwe na yakikwama waihoji bodi nakutoa ushauri zaidi nini kifanyike.