
Nchini Sudan Kusini, wakazi wa jiji la Akobo – lililoko mpakani na Ethiopia, katika sehemu ya mashariki ya Jimbo la Jonglei – wametoroka makazi yao kuanzia Jumamosi, Machi 7 hadi Jumapili, Machi 8, 2026. Likiwa limeshikiliwa na kundi la waasi la Makamu wa Rais Riek Machar, jiji hilo, katika wiki za hivi karibuni, lilikuwa kimbilio la zaidi ya watu 40,000 waliokimbia makazi yao.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Juba, Florence Miettaux
Mapigano yameongezeka tangu mwisho wa mwezi wa Desemba 2025 kati ya vikosi vya Rais Salva Kiir na vile vya upinzani katika eneo hili la kaskazini mwa Jonglei. Siku ya Ijumaa, Machi 6, jeshi lilitoa makataa ya saa 72 kuamuru Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, na raia kuondoka katika eneo hilo. Wakati walinda amani wa Umoja wa Mataifa walibaki katika jiji hiloi, wakazi walianza kutoroka makazi yao, na mji huo ulikuwa tupu kufikia adhuhuri Jumapili, Machi 8.
Wanawake na watoto waliokuwa wametafuta hifadhi huko Akobo waliamua kukimbia kwa miguu, wakiwa wamebeba mali zao vichwani. Makataa hayo yalimalizika Jumatatu, Machi 9, lakini jeshi la serikali lilikuwa tayari limekaribia mji huo siku ya Jumamosi. Mapigano yalianza wakati huo na kuendelea hadi Jumapili asubuhi magharibi mwa Akobo, na kuzua hofu ya shambulio kubwa dhidi ya mji huo.
Kulingana na viongozi wa eneo hilo, ndege mbili ziliondoka Akobo siku ya Jumapili asubuhi kuwahamisha wafanyakazi wa misaada kwenda Juba. Wakati huo huo, wakazi wanakimbilia Ethiopia katika mazingira mabaya. “Watu hawana pa kwenda, kwani tayari wamekimbia vijiji vyao,” ameelezea Sam Koang Malual, mwandishi wa habari wa eneo hilo. Lakini hofu ya mapigano mapya imewalazimu kukimbia, licha ya ukosefu wa misaada ya kibinadamu upande wa pili wa mpaka.
“Hali mbaya”
Makataa ya jeshi la Sudan Kusini yamewaweka waliokimbia makazi yao katika hofu. “Familia zinaondoka na mali chache sana na zinalazimika kutembea umbali mrefu sana katika mazingira magumu. Familia nyingi hizi tayari zimekimbia makazi yao, kwa hivyo hali hii inasababisha wakaazi kukumbaya mabaya yaliyotokea siku za nyuma,” anasema Sam Koang Malual, mkurugenzi wa kituo cha redio ya jamii Akobo FM.
Susan Tab, mfanyakazi wa shirika moja la kutoa msaada nchini Sudan Kusini, hakuwa na chaguo ila kuondoka mji huo: “Kinachonitia wasiwasi zaidi ni wagonjwa na waliojeruhiwa; hawana pa kwenda.”
Shirika lisilo la kiserikali la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) liliwahamisha wafanyakazi wake Jumamosi, Machi 7, kwa mara ya pili ka kipindi cha miezi miwili. Matokeo ya shambulio hili jipya la kijeshi yatakuwa makubwa, kulingana na Christophe Garnier, mwakilishi wa MSF nchini Sudan Kusini: “Tunazungumzia zaidi ya watu 100,000 ambao wanaweza kukimbia, wakiwemo wakazi wa Akobo na waliokimbia makazi yao. Kwa hivyo popote wanapoenda, itasababisha hali mbaya. Watu hawa wana hatari ya kukabiliwa na aina zote za vurugu na watapata shida kubwa kupata huduma ya afya, makazi, na ulinzi. Kwa hivyo labda tutakabiliwa na hali mbaya.”
MSF inatumai kwamba jeshi litafikiria upya uamuzi wake wa kushambulia Akobo.
Kuhusu ujumbe wa Umoja wa Mataifa, bado haujatoa jibu rasmi kwa amri ya serikali ya kufunga kambi yake huko Akobo, lakini vyanzo kadhaa vinabainisha kwamba walinda amani wa Umoja wa Mataifa hawana nia ya kuondoka.