Maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Wanawake Duniani yamebeba kauli mbiu ya kimataifa isemayo “Haki, Usawa na Hatua Madhubuti kwa Wanawake na Wasichana Wote.” Kauli hii inaenda sambamba na wazo la “Give to Gain” au kwa Kiswahili “Kutoa ndiko Kupata,” dhana inayosisitiza kuwa mafanikio na ustawi wa jamii huanza pale mtu anapochukua hatua ya kutoa mchango wake kwa wengine.

Kwa mtazamo mpana, kauli hii inaibua swali muhimu: ina maana gani kwa mwanamke na msichana wa Kitanzania katika mazingira ya sasa ya kijamii, kiuchumi na kielimu? Jibu lake linafungua mjadala mpana kuhusu wajibu wa jamii, serikali na wanawake wenyewe katika kujenga mustakabali wenye usawa na haki.

Kwa miaka mingi, wanawake wa Tanzania wamepiga hatua katika nyanja mbalimbali. Kuongezeka kwa idadi ya wasichana wanaopata elimu, wanawake kushika nafasi za uongozi na kuingia katika sekta za biashara na ubunifu ni ishara ya maendeleo.

Hata hivyo, bado zipo changamoto kama ukosefu wa fursa sawa za kiuchumi, mila kandamizi na vikwazo vya kijamii vinavyowazuia wanawake wengi kufikia uwezo wao kamili.

Katika mazingira hayo, dhana ya “kutoa ndiko kupata” inakuwa na umuhimu mkubwa. Inahimiza wanawake na jamii kwa ujumla kuwekeza katika maendeleo ya wanawake na wasichana kupitia elimu, ujuzi, malezi bora na fursa za kiuchumi. Kwa kufanya hivyo, manufaa yake hayarudi kwa mtu mmoja tu bali kwa jamii nzima.

Mtaalamu wa masuala ya jinsia, Dk Amina Hassan anasema kauli mbiu hiyo inaonyesha kuwa usawa wa kijinsia haupatikani kwa maneno pekee bali kwa vitendo vinavyoonekana.
kwa kuali hiyo, ni wazi kuwa tunaposema haki na usawa kwa wanawake na wasichana, inamaanisha kutoa mazingira yanayowawezesha kupata elimu bora, ajira na nafasi za uongozi kwa wanawake hapa nchini. Inamana Jamii ikitoa fursa hizi, matokeo yake ni maendeleo ya taifa zima.

Kwa mtazamo wangu, uwekezaji kwa mwanamke una athari kubwa kwa familia na jamii. Mwanamke akipata elimu na kipato, uwezekano wa familia yake kupata lishe bora, huduma za afya na elimu kwa watoto huongezeka.

Hivyo, kile kinachoonekana kama kutoa kwa mwanamke kinageuka kuwa faida kwa familia na Taifa kwa ujumla.

Lakini kwa mtazamo chanya ninaouona mimi, kauli inayosema wanawake ni nguvu muhimu katika uchumi wa nchi, inapaswa itambulike na wanawake wote nchini.

Kwamba wanapopata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, uzalishaji huongezeka na kipato cha taifa hukua. Hivyo, kutoa rasilimali na fursa kwa wanawake si hisani, bali ni uwekezaji wenye tija.

Kwa msichana wa Kitanzania, kauli ya “kutoa ndiko kupata” inaweza kutafsiriwa katika njia nyingi. Kwanza ni katika elimu. Msichana anapojituma katika masomo, anatoa juhudi na muda wake kwa ajili ya kujenga mustakabali wake. Matokeo yake ni kupata maarifa, ujuzi na fursa za maisha yake bora ya baadaye.

Lakini hata katika mshikamano wa wanawake wenyewe. Wanaposhirikiana, kusaidiana na kuinuana, wanajenga nguvu ya pamoja inayoweza kubadilisha jamii.

Mfano wa vikundi vya akiba na mikopo maarufu kama Vicoba, umeonyesha jinsi wanawake wanavyoweza kusaidiana kifedha na kuboresha maisha yao.

Hivyo kila mwanamke anapaswa kutambua kwamba mshikamano huo ni nguzo muhimu katika kuendeleza dhana ya kutoa na kupata.
Wanawake wanaposhirikishana uzoefu, maarifa na mitandao ya kibiashara, wanasaidiana kupunguza changamoto wanazokutana nazo. Hiyo ndiyo maana halisi ya kutoa kwa lengo la kupata maendeleo ya pamoja.

Hivyo wazazi wanapaswa kutoa malezi yanayowapa wasichana nafasi sawa na wavulana. Walimu wanapaswa kutoa elimu inayowahamasisha wasichana kujiamini na kuthubutu kuingia katika taaluma mbalimbali, ikiwamo sayansi na teknolojia.

Serikali nayo inapaswa kuendelea kuweka sera na mipango inayolinda haki za wanawake na kuondoa vikwazo vya kijinsia.

Hata hivyo, wataalamu wanasema hatua hizo zinahitaji kuendelea kuungwa mkono na mabadiliko ya mitazamo katika jamii.

Kwa maana hiyo, wakati Tanzania ikiendelea kuadhimisha siku hii ndani ya mwezi huu wa tatu, falsafa ya “kutoa ndiko kupata” inatukumbusha kuwa maendeleo ya kweli huanza pale tunapokuwa tayari kuchangia kwa ajili ya wengine.

Kwa kufanya hivyo, si tu kwamba tunawainua wanawake na wasichana, bali pia tunajenga jamii imara, yenye usawa na yenye matumaini kwa vizazi vijavyo.

0713235309

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *