Istanbul, Uturuki. Meneja wa Liverpool, Arne Slot, ameilaumu timu ya waamuzi kufuatia kipigo cha bao 1-0 walichopata kutoka kwa Galatasaray katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wa hatua ya 16 bora uliochezwa jijini Istanbul, Uturuki jana Machi 10, 2026.

Liverpool ilijikuta ikipoteza mchezo huo kwa bao la kipindi cha kwanza la Mario Lemina, matokeo ambayo yanaiacha timu hiyo katika wakati mgumu kuelekea mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa Anfield.

Hata hivyo, Slot ameonesha kutoridhishwa na maamuzi ya refa, akidai kuwa Liverpool ilipaswa kupewa mkwaju wa penalti katika kipindi cha pili baada ya beki wake Virgil van Dijk kuvutwa jezi ndani ya eneo la hatari.

Tukio hilo pia lilifuatiwa na kufutwa kwa bao la Ibrahima Konaté kutokana na kugusa mpira kwa mkono.

Slot amesema tofauti ya uchezeshaji kati ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya ni kubwa.

Kocha wa Liverpool, Arne Slot (wakwanza kulia), katikati ni beki wa Klabu hiyo, Ibrahim Konate wakati wakijaribu kuzungumza na mwamuzi, Jesús Gil Manzano baada ya kukataa bao katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Galatasaray. Picha na Mtandao

“Katika Ligi Kuu England mambo mengi yanaruhusiwa kuliko Ligi ya Mabingwa. Ndiyo maana nilishangaa kuona tukio lile halikutolewa penalti,” amesema Slot.

Ameongeza kuwa mwamuzi alikuwa akitoa faulo kwa urahisi kwa Galatasaray, lakini ulipofika wakati ambao mchezaji wa Liverpool alipofanyiwa madhambi, hakuchukua hatua.

Kocha huyo pia amekiri kuwa Liverpool ilipoteza nafasi nyingi za kufunga katika mchezo huo, huku akiwapongeza wapinzani wao kwa kutumia vizuri nafasi chache walizopata.

“Ni uwanja mgumu kucheza, lakini unapokuwa tayari umefungwa bao 1-0 inakuwa ngumu zaidi. Hata hivyo, huu bado ni mchezo wa hatua mbili,” amesema Slot.

Kocha wa Liverpool, Arne Slot, wakati akiongea na wanahabari baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Galatasaray kumalizika. Picha na Mtandao

Meneja huyo anaamini mambo yatakuwa tofauti katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Anfield, akitegemea sapoti kubwa ya mashabiki wa Liverpool.

“Mchezo unaofuata hautachezwa hapa bali Anfield, na mashabiki wetu wanaweza kutengeneza mazingira kama haya au hata zaidi. Tuna nafasi ya kurekebisha makosa yetu,” amesema.

Liverpool sasa italazimika kushinda kwa tofauti ya mabao mawili katika mchezo wa marudiano ili kujihakikishia kusonga mbele katika michuano hiyo mikubwa barani Ulaya. 

Mshambuliaji wa Newcastle, Barnes, wakati akifunga bao katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyomalizika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Barcelona. Picha na Mtandao

Newcastle yabanwa nyumbani

Katika mchezo mwingine uliopigwa katika dimba la St. Jame’s Park, England, wenyeji Newcastle walilazimishwa sare ya bao 1-1 na Barcelona.

Newcastle United ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya 86 kupitia kwa Barnes ambaye alimalizia krosi kutoka kwa Jacob Murphy.

Hata hivyo, matumaini ya Newcastle kuondoka na ushindi yalikatishwa katika dakika za majeruhi baada ya kiungo mshambuliaji wa Barcelona, Dani Olmo kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na beki Malick Thiaw, hali iliyosababisha mwamuzi kuruhusu mkwaju wa penalti ambao ulizamishwa wavuni na Lamine Yamal.

Mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez, akifunga bao baada ya kipa wa Spurs, Antonin Kinsky, kufanya makosa alipokuwa akitaka kuondoa mpira katika eneo la hatari katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao

Atletico yaibuluza Tottenham

Katika Uwanja wa Metropolitano, Madrid, Hispania ilishuhudiwa vijana wa kocha Diego Simeone wakipeleka kipigo cha fedhea baada ya kuifunga Tottenham mabao 5-2.

Mabao ya Atletico yalifungwa na Julian Alvarez ambaye aliyepachika mawili huku mengine yakifungwa na Antoine Griezmann, Marcos Llorente pamoja na Robin Le Normand wakati kwa upande wa Spurs mabao yao yalifungwa na Pedro Porro na Dominic Solanke.

Baadhi ya wachezaji wa Bayern Munich, wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 6-1 walioupata dhidi ya Atalanta katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao

Bayern yatamba ugenini

Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich nao walitoa kipigo kizito cha mabao 6-1 ugenini dhidi ya Atalanta.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa New Balance, Bayern iliandika bao la uongozi dakika ya 12 kupitia kwa Josip Stanisic kabla ya Michael Olise kufunga lingine dakika ya 22 wakati mabao mengine yakifungwa na Serge Gnabry ambaye alifunga la tatu dakika ya 25, mshambuliaji Nicolas Jackson aliandika bao la nne kabla ya Michael Olse kufunga lingine kisha Jamal Musiala kuhitimisha kalamu ya ushindi kwa kupachika bao la sita dakika ya 67 wakati lile la kufutia machozi kwa upande wa Atalanta likifungwa dakika za mwishoni na Mario Pasalic.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *