Nchini Afrika Kusini, wanajeshi wametumwa kulinda usalama katika maeneo yanayoaminiwa kuwa na usalama mdogo jijini Johannesburg.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hatua hii inakuja, kufuatia kauli ya rais Cyril Ramaphosa kuwa changamoto za kiusalama jijini Johannesburg, zimekuwa tishio kubwa kwa nchi hiyo.
Magari ya kijeshi yameonekana, yakipiga doria katika mitaa ya Magharibi mwa jiji hilo, baada ya rais Ramaphosa mwezi uliopita, kuagiza wanajeshi kusaidia kurejesha usalama.
Wakiwa wamevalia magawanda ya kijeshi na kujihami, wanajeshi hao wakiwa na polisi wanafanya msako wa nyumba kwa nyumba, wakitafuta silaha na dawa za kulevya.
Maeneo ya Riverlea na Westbury ambayo yameshuhudia visa vingi vya mauaji ambapo watu wanapigwa risasi, ndio yanayolengwa zaidi na operesheni hiyo ya kijeshi.
Hata hivyo, baadhi ya wakaazi hawaamini iwapo kutakuwa na mabadiliko yoyote, licha ya rais Ramaphosa kutangaza kuwa operesheni hiyo itadumu kwa mwaka mmoja na mbali na Johannerburg, wanajeshi hao pia watakuwa katika mikoa tisa ikiwemo Cape Magharibi.