
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, ameishukuru serikali na wananchi wa India kwa kuonesha mshikamano na watu wa Iran, akisema kuwa Iran daima imekuwa ikiiheshimu India kama rafiki na mshirika muhimu wa kiuchumi.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, Rais Pezeshkian na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, wamefanya mazungumzo ya simu wakijadili matukio ya hivi karibuni kufuatia vita vya kichokozi vinavyoendelezwa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran pamoja na athari zake.
Katika mazungumzo hayo, Rais Pezeshkian amesisitiza kwamba wakati Iran ilikuwa katika njia ya mazungumzo na Marekani ili kutatua masuala kupitia diplomasia, ndipo shambulio la kikatili la Marekani na utawala wa Kizayuni lilipotokea. Amesema kitendo hicho cha uvamizi kilikiuka wazi kanuni za kimataifa na sheria za kibinadamu.
Rais wa Iran amesema kuwa uvamizi huo umesababisha kuuawa shahidi kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, makamanda waandamizi wa kijeshi, wanafunzi 168 wasio na hatia waliokuwa katika shule moja ya wasichana mjini Minab, mbali na idadi kubwa ya raia ambao hadi sasa wameuawa shahidi. Ameongeza kuwa Kiongozi huyo shahidi, mbali na nafasi yake ya uongozi wa kisiasa, alikuwa pia kiongozi wa kiroho wa Waislamu duniani, na kwa msingi huo kulipiza kisasi damu yake ni haki ya kimsingi ya Umma wa Kiislamu.
Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikuanza vita na haina nia ya kuendeleza mapigano, lakini kwa mujibu wa haki ya kujilinda, imelenga vituo vya kijeshi vya Marekani katika baadhi ya nchi za eneo ambavyo vilitumika kama chanzo cha mashambulizi.
Rais huyo pia amelaani vikali mauaji ya watu wasio na hatia yanayofanywa na utawala wa Kizayuni, akiyataja kuwa mfano dhahiri wa ugaidi wa kiserikali. Amesema Iran haina nia ya kuzusha ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati, na licha ya mashambulizi ya hivi karibuni yaliyolenga miundombinu ya Iran, Tehran bado imejizatiti kuendeleza ushirikiano na India pamoja na nchi rafiki kupitia mifumo ya kimataifa kama vile BRICS na Shirika la Ushirikiano la Shanghai.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa BRICS kuchukua nafasi hai katika kulinda amani, utulivu na usalama wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ameeleza wasiwasi mkubwa wa nchi yake kuhusu kuongezeka kwa mvutano katika Mashariki ya Kati, akisisitiza kuwa India ni rafiki wa Iran. Amesema New Delhi itafanya juhudi zake zote kuendeleza njia ya diplomasia, akibainisha kuwa kuongezeka kwa mapigano hakutamnufaisha upande wowote.
Modi pia amebainisha masikitiko yake kwa kuzuka kwa vita katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, na akatumaini kwamba mwaka mpya wa jua wa Kiajemi na sikukuu ya Nowruz utaleta ujumbe wa utulivu, amani na uthabiti katika eneo huku akisisitiza kwamba masuala yanapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo na diplomasia.