Liverpool, England. Meneja wa Liverpool, Arne Slot amesema kwamba kumkosa nyota wake Alexander Isak kwa muda mrefu kumechangia timu yake isifanye vizuri msimu huu.

Timu hiyo inaonekana kuelekea kushindwa kutetea taji la Ligi Kuu England (EPL) msimu huu kwa vile imezidiwa kwa tofauti ya pointi 19 na vinara Arsenal huku ikibakiza mechi rıza kabla ya msimu kumalizika ambapo kwa sasa ina pointi 48 huku ikiwa nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi.

Liverpool pia ipo katika wasiwasi wa kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kupoteza mechi ya kwanza ya hatua ya 16 Bora ugenini dhidi ya Galatasaray kwa bao 1-0.

Ilitupwa nje katika Kombe la Calabao na Kombe la FA ndilo pekee ambalo Liverpool imebaki na matumaini ya kulichukua ingawa inaonekana inaweza isiwe rahisi kwa vile imepangwa kukutana na Manchester City katika hatua ya robo fainali.

Na Slot anaonekana kukubaliana na hali halisi kwamba huu ni msimu mgumu kwao huku akiamini changamoto ya majeraha kwa wachezaji wake hasa Isak aliyesajiliwa katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi mwaka jana, imechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya timu yake iyumbe msimu huu.

Isak yupo nje ya uwanja tangu Desemba mwaka jana alipovunjika mguu katika mechi dhidi ya Tottenham Hotspur na Slot anaamini kama mshambuliaji huyo angekuwepo, timu yake sasa hivi ingekuwa moto wa kuotea mbali.

“Na kama ukimkosa Alex (Alexander Isack) manage ndiye usajili mkubwa zaidi tulioufanya.  Tulifanya sajili kadhaa kubwa, lakini huu (wa Isak) ulikuwa mkubwa zaidi,  hilo limekuwa na athari kubwa sana kwetu.

“Angalia pia kila klabu, tazama ni mabao mangapi tumefunga msimu huu. Hiyo ni idadi ndogo sana kwa timu, lakini pia kwa washambuliaji wetu.

“Ndogo sana, namaanisha ukilinganisha na viwango tulivyozoea. Nadhani ukiangalia washambuliaji wa Liverpool katika miaka 10 iliyopita, mabao yalikuwa mengi zaidi. Na bila shaka inakuwa na athari pale mmoja wa washambuliaji tuliomsajili kwa ajili ya kufunga mabao anapokuwa ameumia,” alisema Slot.

Hata hivyo, Isak anatarajiwa kuanza hatua za kurejea uwanjani mwezi ujao, lakini Slot amesisitiza kwamba kusiwekwe matarajio makubwa katika urejeo wa mshambuliaji huyo wa Sweden aliyenunuliwa kwa Pauni 125 milioni akitokea Newcastle United.

“Tena inanibidi nivunje sherehe. Tuseme atarejea mwanzoni mwa Aprili, lakini amekuwa nje kwa miezi mitatu na nusu. Hajafanya mazoezi na timu katika kipindi chote hicho.

“Mara ya mwisho aliporudi kutoka majeruhi kama hayo, ilimchukua muda kurejea kwenye kiwango chake.

“Natazamia sana kumpata tena, lakini tusiweke matarajio kupita kiasi kiasi kwamba mara tu anapoingia uwanjani awe tayari kwenye kiwango kilekile tulichotarajia baada ya kumlipia fedha nyingi,” alisema Slot.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *