Dar es Salaam. Baadhi ya wanamuziki wa Bongofleva, katika kuandika, kutayarisha na kurekodi nyimbo zao, huwa wanapata na hata kuchukua mawazo kutoka katika kazi ambazo zilifanya vizuri hapo awali.

Leo tunakupa nyuma ya pazia kwa namna walivyoweza kuandaa baadhi ya kazi zao na hata kujenga chapa zao kupitia wenzao wa kimataifa kama ifuatavyo.

1. Wimbo wa Ngwair ‘Mapenzi Gani’ kutoka katika albamu yake ya pili, Ng’e (2009) akimshirikisha Lady Jaydee, biti yake iliyotayarishwa na Lamar ni sampo ya wimbo wa Whitney Houston, Saving All My Love for You (1985).

2. Kwa kipindi kirefu rapa Mansu-Li amejitambulisha kama ‘Underground King’, licha ya kuwa tayari unajulikana. Hata hivyo, wasanii wengi wa Hip Hop walianza kujiita ‘Underground’ baada ya 50 Cent kutoa wimbo wake, Many Men (Wish Death) (2003).

3. Wimbo wa Stereo ‘Rafiki’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, African Son (2011) akimshirikisha Grace Matata, mdundo wake waliotengenezwa na Duke Tachez umechukua vionjo kutoka katika wimbo, I Against I (2000) wa kundi Jedi Mindi Tricks.

4. Mwimbaji na video vixen wa zamani Bongo, Amber Lulu, aliamua kujipa jina hilo kutokana na mtindo wake wa kunyoa (low cut) na kupaka nywele rangi ambao unafanana na ule wa mwanamitindo Amber Rose, mpenzi wa zamani wa Kanye West.

5. Wimbo wa Nikki Mbishi, Secreto de Amor (2014), na ule wa Young Killer, Secreto (2018), zote zimesampo wimbo (soundtrack) ya tamthilia ya Kihispania, Secreto de Amor (2001) ambayo ni maarufu huko Latin America.

6. Lamar alipata wazo la kuweka kisauti cha kujitambulisha (sign tune) katika kila wimbo alioutengeneza kutoka kwa Diddy. Hapo awali, nyimbo nyingi za Bad Boys Records zilikuwa na utambulisho fulani wenye sauti ya Diddy.

7. Wimbo wa Songa, Picha (2018) uliotayarishwa na Ringle ambaye ni mshindi wa Tuzo za Muziki (TMA) 2023, una vionjo kutoka katika wimbo wa Mariah Carey, Love Takes Time (1990).

8. Rapa Witness baada ya kuimba vizuri wimbo wa Gwiji wa Country Music, Dolly Parton, Jolene (1973), alishauriwa kushiriki shindano la Coca-Cola Popstar East Africa 2004, na baadaye alikuja kushinda.

9. Wimbo wa Nikki Mbishi ‘Kila Siku’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Sauti ya Jogoo (2011), rapa Godzilla ambaye alishirikishwa, amepita na midondoko ya Jay Z kutoka katika ngoma, Run This Town (2009) akiwa na Kanye West na Rihanna.

10. Wimbo wa Vanessa Mdee ‘Bambino’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Money Mondays (2018) akimshirkisha Reekado Banks wa Nigeria, una melodi na mistiri ya wimbo wa Whitney Houston, My Love Is Your Love (1998).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *