Dar es Salaam. Wapo wanawake waliopitia manyanyaso ya kijamii na kifamilia, huku wengine wakageuzwa kichekesho kutokana na muonekano wa miili yao. Hata hivyo, baada ya kusimama imara na kuzitumia changamoto kama fursa, sasa wana ushawishi mkubwa na nguvu ndani na nje ya nchi.
Siyo Tanzania pekee ndiko kunakotokea unyanyasaji kwa wanawake. Kabla dunia haijamfahamu Oprah Winfrey, alipitia unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa watu wa karibu naye, lakini akayatumia matukio hayo kama kipaza sauti cha kugusa maisha ya wengine.
Oprah, aliyezaliwa Januari 29, 1954 huko Mississippi, Marekani, akiwa na umri wa miaka 14 alipata ujauzito na mtoto wake alifariki dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa. Mwanzoni mwa kazi yake ya utangazaji alikumbana na ubaguzi wa rangi na jinsia, na aliwahi kuondolewa katika kazi ya usomaji wa habari kwa madai kuwa hafai kuonekana kwenye kamera. Pamoja na hayo yote, hakukata tamaa na kwa sasa anahoji watu maarufu na viongozi wakubwa duniani.
Baadhi ya watu aliowahi kuwahoji ni Meghan Markle na Prince Harry wanaotoka katika familia ya kifalme ya Uingereza, Michelle Obama mke wa rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, na wengine wengi.
Mwanamama huyo alianzisha mtindo wa mazungumzo uliomfanya awe maarufu duniani kupitia kipindi chake, The Oprah Winfrey Show, ambacho kimekuwa msaada kwa wanawake wanaopitia vitendo vya unyanyasaji na ubaguzi.
Kibongobongo, Mwananchi linakuletea baadhi ya wanawake ambao hawakukubali manyanyaso na kuchekwa kuue ndoto zao, bali walisimama imara na sasa wana nguvu kubwa katika jamii na wamekuwa mfano wa kuigwa.
Rose Mhando
Malkia wa nyimbo za injili Tanzania, Rose Mhando, katika mahojiano mbalimbali aliyowahi kufanya aliwahi kusimulia juu ya manyanyaso aliyowahi kupitia. Hata hivyo, hakuyaruhusu yamrudishe nyuma na sasa ni mwanamke wa shoka na mwenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya nchi.
Hiki ni kisa mojawapo kati ya vingi vilivyowahi kumuumiza: “Kwetu tupo sita, mimi ni wa mwisho. Naeleza hivyo ili watu wamfahamu Rose ni nani, siyo Rose maarufu. Ukiachana na magonjwa niliyopitia, kilichowahi kuniumiza ni kipindi baba yangu alipofariki. Niliitwa na ukoo wa baba yangu na waliniambia huyo hakuwa baba yako mzazi, kwa hiyo huwezi kurithi kitu chochote.
“Ndiyo maana sikuwahi kuthubutu kuwaambia watoto wangu huyu siyo baba yako. Hata angekuwa na mguu mmoja, atabakia kuwa baba yao, ili mradi tu wamwone kwamba huyu ndiye baba yao. Maana mimi wa kwangu simjui hadi leo.
“Siku tatu baada ya mazishi ndugu yangu mkubwa akauza nyumba, mimi na mama tukaambiwa tuondoke na hatukujua tunaenda wapi. Siku hiyo mvua ilinyesha sana na ilitunyeshea wakati tunatembea njiani. Ilipofika jioni tukajisogeza kwenye mti tukalala hapo. Kuna mtu alikuwa anamfahamu mama, alikata miti na kutujengea kibanda cha nyasi tukawa tunaishi hapo. Nafahamu kuna watu wengi ambao wanapitia magumu, lakini wasije wakakata tamaa katika maisha yao.”
Tausi Mdegela
Muigizaji wa filamu, Tausi Mdegela anasema haikuwa safari rahisi kwa Watanzania kukifahamu kipaji chake.
Alipitia dharau na manyanyaso, lakini havikumkatisha tamaa. Badala yake alijua hatima ya maisha yake lazima apambane mwenyewe.
“Kabla ya kuanza kuigiza kuna mtu nilimuomba anipe nafasi ili nionyeshe kipaji changu. Baada ya kufika eneo aliloniambia tuonane akapiga simu. Nilipopokea akaniambia, ni wewe? Nikamjibu ndiyo. Akasema hakuna kazi. Nilijisikia vibaya, ila niliamini ipo siku nitafanikiwa,” anasema Tausi na kuongeza:
“Kuna wakati hata binti yangu wenzake walikuwa wanamwambia mama yako ni mfupi halafu kadogo. Nilimwambia mwanangu mimi siumwi na nakupatia kila kitu unachokitaka, halafu kawaambie ndiyo mama yangu mfupi ila ni maarufu na ananipa kila ninachokitaka. Hawakurudia tena kumwambia.
“Nina marafiki zangu warefu huwa wananiambia Tausi wewe ni imara ila kuna vitu vingine tuwe tunakusaidia. Mimi napambana, kuna wakati najisahau kama mfupi labda ufike muda wa kufungua mlango ndiyo nakumbuka siwezi.”
Msanii wa tamthilia ya Jua Kali, Hellen Herman ‘Loveness’, kuna wakati akiposti picha au video zake mtandaoni, mfano Instagram, kuna watu wanamtupia maneno ya kejeli kutokana na muonekano wa mwili wake wa unene. Hata hivyo, hilo halijawahi kumkatisha tamaa, badala yake anaendelea mbele na kipaji chake.
“Najikubali kama nilivyo. Sababu ya kuigiza ni kwamba nilikuwa nimeposti video yangu kwenye status, kuna mtu akaiona akaiposti Instagram. Huko ndiko Lamata alikoniona, akanitumia ujumbe DM. Baada ya kukutana akanishawishi nianze kuigiza. Watu wanaonisema kuhusu mwili wangu sijali na wala siwazi. Najikubali na kujiamini,” anasema Loveness.
Loveness Tarimo
Loveness Tarimo ni mkufunzi wa mazoezi na Miss Mtunisha Misuli aliyetwaa taji hilo 2019 katika shindano lililofanyika Tanzania.
Anasema muonekano wake unachukuliwa kwa hisia tofauti na jamii, lakini hilo halimsumbui.
“Nakumbuka wakati nakwenda Kenya kwenye mashindano ya Miss Mtunisha Misuli miaka kadhaa iliyopita, nilienda Sinza kununua hereni. Muuzaji alikuwa ni mwanamke, alikataa kuniuzia akidhani ni mwanaume. Niliumia lakini ilibidi nikubaliane na hali halisi,” anasema Loveness na kuongeza:
“Mimi ni mkufunzi wa mazoezi, ni kazi inayonipa kipato. Siwezi kuteteleka na kurudi nyuma kwa sababu ya mitazamo ya watu kuhusu mwili wangu. Kwa nchi za nje, Miss Mtunisha Misuli ni kitu cha kawaida tofauti na hapa kwetu.
“Kama kuna binti ana ndoto zake asiogope kusemwa wala kuchekwa. Anapaswa akipambanie kile anachokiona kitabadilisha maisha yake.”
Msanii wa tamthilia ya Jua Kali, Wanswekula Zacharia ‘Dora’, pamoja na kupitia changamoto nyingi ikiwemo ugonjwa wa sickle cell, hiyo haikuwa sababu ya kushindwa kuzipambania ndoto zake. Sasa ni mwanamke mwenye nguvu na ushawishi na amekuwa akishiriki katika majukwaa mbalimbali ya shughuli za kijamii.
“Kwa sasa sishangai mtu kuniangalia, nachukulia kama ameniona mtu maarufu. Zamani kabla sijapona sickle cell nilikuwa na mwili mdogo sana, ila kwa sasa najivunia mwili wangu nauona mkubwa. Mabinti wasikate tamaa, lazima wapambane kufanya kile wanachokiamini na wajue jamii inawategemea,” anasema Dora.