Baraza la Mabunge ya Jumuiya ya Makubaliano ya Usalama wa Pamoja (CSTO) limetoa taarifa ya pamoja likitangaza mshikamano wake na serikali pamoja na watu wa Iran katika kukabiliana na hujuma za kijeshi za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Limesema: “Matumizi au tishio la nguvu dhidi ya nchi huru ni jambo lisilokubalika na kitendo hicho ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.”

Baraza la Bunge la Jumuiya ya Makubaliano ya Usalama wa Pamoja (CSTO) limesema katika taarifa hiyo kuwa: “Tunasisitiza ulazima wa kudhaminiwa mamlaka ya Iran, usalama na umoja wa ardhi yake dhidi ya hujuma za kijeshi za Marekani na Israel na kutoa rambirambi zetu za dhati kwa familia za wahanga.” Taarifa hiyo imeelezea wasi wasi mkubwa wa mabunge ya nchi wanachama wa CSTO ambazo ni Armenia, Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Russia, na Tajikistan kutokana na kushadidi mivutano katika eneo, inayosababishwa na vitendo vya kichochezi vinavyofanywa na vikosi vya nje vinavyolenga kuvuruga Iran na kuongeza: “Tunatangaza mshikamano na uungaji mkono wetu kwa serikali na wananchi wa Iran.”

Baraza la Mabunge ya Jumuiya ya Makubaliano ya Usalama wa Pamoja limesisitiza katika taarifa hiyo kwamba: “Tunachukulia matumizi ya nguvu kuwa jambo lisilokubalika kabisa na tunataka utatuzi wa migogoro iliyopo ufanyike kwa njia za amani tu na kwa msingi wa mazungumzo, kuheshimiana na kuzingatiwa maslahi ya pande zote, kwa kutilia maanani sheria na kanuni zinazotambulika kimataifa ikiwa ni pamoja na Hati ya Umoja wa Mataifa.” Taarifa hiyo imeendelea kusema: “Tunautaka Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama zichukue hatua za haraka kwa lengo la kukabiliana na uvunjifu wa amani na usalama wa kimataifa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *