Vikosi vya jeshi la Yemen vimetangaza kwamba vimeshambulia shabaha nyeti kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) kwa makombora ya balestiki.

Vikosi vya wapiganaji wa Ansarullah nchini Yemen vimetoa taarifa mapema leo Jumamosi na kutangaza kwamba vimefanya operesheni ya kwanza ya kijeshi dhidi ya Israel kwa kurusha makombora ya balestiki dhidi ya malengo nyeti ya kijeshi ya utawala huo, kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Taarifa hiyo imesema: “Katika utekelezaji wa kile kilichosemwa katika taarifa ya awali ya Jeshi la Yemen kuhusu kuingilia kati moja kwa moja kijeshi ili kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kambi ya Muqawama nchini Lebanon, Iraq na Palestina, na kwa kuzingatia kuendelea mashambulizi ya kijeshi yanayolenga miundombinu na kufanya uhalifu na mauaji dhidi ya ndugu zetu huko Lebanon, Iran, Iraq na Palestina, tumefanya operesheni yetu ya kwanza ya kijeshi kwa kurusha makombora ya balestiki dhidi ya malengo nyeti ya kijeshi kusini mwa utawala wa Kizayuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.”

Katika muktadha huo, Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa Jeshi la Yemen, amesema: “Operesheni zetu zitaendelea hadi malengo yaliyotangazwa yatakapotimizwa na hadi uchokozi katika pande zote za Muqawama utakapokoma.”

Awali Yahya Saree alikuwa amesema kuwa uchokozi wa kikatili unatekelezwa na tawala hasimu za Marekani na Israel, ambazo zinalenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mhimili wa Jihad na Muqawama, pamoja na Umma mzima wa Kiislamu, kwa lengo la kuanzisha “Israel Kubwa,” chini ya kivuli cha mpango wa “kubadilisha Mashariki ya Kati.”

Aliongeza kuwa: Jeshi la Yemen halitaruhusu Bahari Nyekundu kutumiwa kutekeleza operesheni za uhasama za Marekani na Israel dhidi ya Iran au dhidi ya nchi yoyote ya Kiislamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *