Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba ametoa ufafanizi rasmi kuhusu hatma ya eneo la Coco Beach, akisisitiza kuwa halitauzwa kwa mwekezaji yeyote bali maboresho yatafanyika kwa manufaa ya wananchi waliopo katika eneo hilo.
Amesema hayo leo, Machi 29, 2026, alipotembelea eneo la Coco Beach jijini Dar es Salaam na kuzungumza na wajasiriamali wadogo wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo na kusikiliza kero zao mbalimbali.
“Coco Beach haiuzwi. La kwanza niwaondolee hofu—hapauzwi, wala hakuna mwekezaji mwingine zaidi yenu nyinyi wenyewe. Hakuna atakayekuja kutoa maelekezo zaidi ya yale yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hapa hapauzwi,” amesisitiza.
Aidha, Dkt Mwigulu amesema Serikali itaendelea kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wananufaika na maboresho yanayofanyika katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Dkt Mwigulu amewataka watendaji wa Manispaa ya Kinondoni, akiwamo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Biashara pamoja na watendaji wengine, kubadili mtindo wa utendaji kazi kwa kuwafuata wananchi moja kwa moja badala ya kuwasubiri ofisini.
“Ninatoa agizo kwa Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Afisa Biashara pamoja na watendaji wengine—msikae ofisini tu. Tokeni mkazungumze na wananchi hawa moja kwa moja pale wanapokuwa na masuala yanayowahusu,” amesisitiza.
(Feed generated with FetchRSS)