
Dar es Salaam. Uzee ni hatua ambayo wengi huiogopa au kuichukulia kama mwisho wa mvuto na furaha ya maisha, lakini kwa Mama Mobetto, hali ni tofauti kwani anaamini ni mwanzo wa sura mpya yenye heshima na thamani kwa mhusika.
Mama huyo mzazi wa mwanamitindo wa Bongo, Hamisa Mobetto, maarufu kama Mama Mobetto ameiambia Mwananchi kuwa anauona uzee ni nafasi yake kuwa bibi mwema ndani ya familia.
Akiwa mlezi wa karibu wa wajukuu zake wawili ambao ni watoto wa Hamisa, Mama Mobetto amesema kuwa jukumu hilo linampa nguvu na kumfanya ajione mwenye thamani zaidi kadri anavyoendelea kukua kiumri.
Katika mahojiano yake, ameeleza kuwa anachokiweka mbele ni namna atakavyokumbukwa na wajukuu wake akisisitiza hataki kuwa bibi wa kawaida, bali wa kipekee.
“Ninapofikiria uzee siuoni kama mwisho wangu, bali naona kama nafasi ya kuwa bora zaidi, nataka wajukuu zangu wanione kama mtu wa mfano, mtu ambaye aliwalea kwa mapenzi, aliwajenga kimaadili na kuwaacha na kitu cha kujivunia,” amesema Mama Mobetto.
Ameendelea kusema kuwa ndoto yake kubwa ni kuhakikisha kuwa hata atakapokuwa mzee, bado ataendelea kuwa mwanamke mwenye kujiamini, heshima na mvuto.
“Natamani siku moja wajukuu zangu waje kuniangalia na kusema kwa fahari kuwa walikuwa na bibi wa kipekee sana, si kwa sababu ya maneno tu bali kwa matendo niliyowaonesha katika maisha yao,” ameongeza.
Mama huyo amewataka wanawake wengine kutouogopa uzee akisisitiza kuwa kila hatua ya maisha ina uzuri wake, na kwamba kuwa mama au bibi ni nafasi adhimu ya kuacha alama chanya kwa kizazi kijacho.