RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika uhifadhi na uimarishaji wa maeneo ya kihistoria kwa lengo la kulinda utamaduni na kukuza uchumi wa Zanzibar.

Akizungumza Ikulu Zanzibar Aprili 1, 2026, alipokutana na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Marjo Crompvoets, Rais Mwinyi amesema juhudi hizo zinahusisha pia ukarabati wa Sinema ya Majestic unaofanyika kwa ushirikiano na Japan kwa lengo la kuhifadhi hadhi yake ya kihistoria na kuongeza matumizi ya kiutamaduni.

Ameishukuru Uholanzi kwa ushirikiano uliopo na kuwahimiza wawekezaji kutoka nchini humo kuja kuwekeza Zanzibar katika sekta za utalii, uchumi wa buluu, viwanda, uvuvi na kilimo. Kwa upande wake, Balozi Crompvoets ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano huo na kuongeza uwekezaji, akieleza kuridhishwa na kasi ya maendeleo ya kiuchumi Zanzibar. SOMA: Wawekezaji Ufaransa Waalikwa Zanzibar

Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi amekutana na Balozi wa Slovakia nchini Tanzania, Ivan Lančarič, ambapo ameonesha utayari wa Zanzibar kushirikiana na nchi hiyo katika sekta za uwekezaji, biashara na utalii. Naye Balozi Lančarič amesema Slovakia inapanga kufungua ubalozi nchini Tanzania pamoja na ofisi ndogo Zanzibar ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji kati ya pande hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *