
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaendelea kuimarisha viwanja vya michezo visiwani humo kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana kupitia sekta ya michezo.
Waziri Riziki ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa viwanja vya michezo katika eneo la Kinyikani, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema ujenzi wa mradi huo unaendelea kuridhisha na kwamba endapo ukikamilika utasaidia kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya michezo nchini.
“Nawapongeza wakandarasi wa mradi huo, kampuni ya Reform Sports, kwa juhudi wanazozifanya katika ujenzi huo ila nataka kuzingatia viwango bora ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa “ amesema.
Pia amewataka wananchi kuilinda na kutunza miundombinu ya michezo inayojengwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Michezo Zanzibar, Amer Mohamed Makame amesema viwanja 17 vya mikoa na wilaya vimejengwa Unguja na Pemba kuimarisha sekta ya michezo.
Amesema, Uwanja wa Kinyikani ni miongoni mwa viwanja vikubwa ambavyo vina miundombinu mbalimbali ya michezo pamoja na mabweni ya wanamichezo wa kike na wa kiume.
Hivyo, amewahimiza wananchi na wadau wa michezo kuvitumia na kuvitunza ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kukuza sekta hiyo.
Naye Katibu wa Shehia ya Kinyikani, Salim Khatib Salim, ameishukuru Serikali kwa kuwaletea miradi ya maendeleo inayowasaidia wananchi, ikiwemo kutoa ajira kwa vijana.