Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo ametangaza neema kwa wakulima wa Idofi, Wilaya ya Makambako ambapo Serikali itatekeleza mradi mkubwa wa umwagiliaji utakaohusisha zaidi ya ekari 1.300.

Amesema Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), imejipanga kuhakikisha wananchi wanatumia rasilimali zilizopo ili kuleta maendeleo endelevu.

“Nimekuja mwenyewe kuwaambia ukweli wa kile kinachotakiwa kufanyika. Ni lazima tukae mkao wa watu tunaojua tunachokitaka,” amesisitiza Waziri Chongolo.

Kwa mujibu wa tathmini ya awali ya wataalamu, mradi huo utahusisha ujenzi wa bwawa la umwagiliaji na uwekaji wa miundombinu ya kisasa itakayowezesha uzalishaji wa mazao mwaka mzima.

Aidha Waziri Chongolo amewahakikishia wananchi kuwa hakuna mkulima atakayepoteza eneo lake kutokana na utekelezaji wa mradi huo.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Makambako, Kenneth Haule amewataka wananchi kujifunza kutoka katika maeneo ambayo tayari yamenufaika na miradi ya Umwagiliaji kama vile Igomelo, Pawaga na Itipingi, ambako uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Usanifu Mhandisi Sadati Kolowa kutoka NIRC amebainisha kuwa ushirikishwaji wa wananchi ni kipaumbele katika miradi yote ya umwagiliaji, kuanzia hatua za awali hadi utekelezaji wake, ili kuhakikisha kunakuwa na uelewa na maridhiano ya pamoja.

Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Njombe, Machage Mwema amesema wananchi watapewa umiliki wa maeneo yao ndani ya mradi huo na watakuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi juu ya matumizi ya ardhi zao.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *