Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limewakamata vijana saba katika Wilaya ya Sumbawanga, huku wawili kati yao wakipandishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita kila mmoja, kwa kudai kuibiwa nyeti zao, jambo ambalo liliwachochea wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuwashambulia wasiokuwa na hatia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Shadrack Masija, amesema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya msako uliofanywa Aprili 6, 2026 kufuatia taharuki zilizochochewa na madai ya wizi wa nyeti, hali iliyosababisha vurugu na kukosekana kwa amani katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo.

Vijana wawili waliohukumiwa, Haruni Willium Mengo (24) mkazi wa Kalambazile na Isack Simon Kaniki (19) mkazi wa Mshani, walimzushia Issa Athuman Kidungwe (56) kutoka Handeni kuwa amewaibia nyeti zao, jambo lililosababisha kushambuliwa na kupata maumivu makali.

Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 8, 2026 na Hakimu Wiligisi Mbunda wa Mahakama ya Mwanzo Kipeta, Wilayani Sumbawanga.

Watuhumiwa wengine watano, Geofrey Dominic (24), Jafari Nebart (25), Huruma Kasonso (18), Constantino Kiatu (26), na Severino Ngonyani (22, wanaendelea kushikiliwa huku taratibu za kisheria zikiendelea ili kufikishwa mahakamani.

#azamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *