ARUSHA: Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan, Tanzania (AKHST) shirika lililo chini ya Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan  (AKDN), kupitia Mradi Mtambuka wa kupambana na saratani kwa Wanawake Afrika Mashariki (EA-CwCP), imetoa vifaa vya tiba ya kemikali vyenye thamani ya Sh milioni 55 ikiwa ni hatua ya kuunga mkono uanzishwaji wa huduma za saratani kwa wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru iliyopo Mkoani Arusha.

Vifaa vilivyotolewa vinajumuisha viti vya kupumzikia wagonjwa , pampu za
kudunga dawa na vifaa vya usalama wa kibaolojia ambavyo vitaboresha utoaji wa huduma za tiba ya kemikali kwa wagonjwa na kuhakikisha usalama wa
wagonjwa na wahudumu wa afya.

Akizungumza leo Jijini Arusha,Katibu Tawala Wilaya ya Arusha , Jacob Rombo ameshukuru kwa mchango wa taasisi ya AKHST katika kujitolea kuimairisha
huduma za saratani nchini na kusema kuwa vifaa hivyo vitaboresha utoaji wa huduma za tiba ya kemikali kuongeza na kulinda usalama wa wahudumu wa afya.

Naye mwakilishi kutoka Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan, Tanzania,Murtazar Mukhtar amesisitiza jukumu la shirika hilo katika kusaidia juhudi za serikali na kuongeza kuwa kupitia uwekezaji katika vifaa, miundombinu, na mafunzo, AKHST itaendelea kujitolea kuimarisha mfumo wa afya na kupanua upatikanaji wa huduma bora nchini.

“Mchango huu ni sehemu ya mkakati mpana wa AKHS Tanzania katika kupambana na saratani na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kupitia uimarishaji wa miundombinu ya afya na kuongeza upatikanaji wa huduma bora nchini.

Mradi Mtambuka wa Kupambana na Saratani kwa Wanawake Afrika Mashariki ni mradi wa kikanda chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD)unaolenga kuimarisha kinga, uchunguzi wa mapema, na matibabu ya saratani za wanawake hasa saratani ya matiti, shingo ya kizazi na chanjo ya HPV kwa wasichana walio katika umri wa miaka 8 hadi 14 katika Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *