MASHINDANO ya urembo ya Miss Tanzania yameingia katika sura mpya baada ya jukumu la kuyaendesha kukabidhiwa rasmi kwa taasisi ya Lamata Village, hatua inayotarajiwa kurejesha hadhi na mvuto wa shindano hilo lenye historia kubwa nchini.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo leo Aprili 14, mwaka huu, Mkurugenzi wa Kampuni ya The Look, Basila Mwanukuzi, amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994, Miss Tanzania imekuwa chachu ya mabadiliko kwa washiriki wake na jamii kwa ujumla.
Amesema washindi wengi wa mashindano hayo wamefanikiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika nyanja mbalimbali, baadhi wakijikita katika tasnia ya sanaa ikiwemo uigizaji, akiwataja warembo waliowahi kushiriki kama Jokate Mwegelo na Aunt Ezekiel. “Ukifuatilia historia ya Miss Tanzania kuanzia mwaka 1994 hadi sasa, utaona jinsi washindi wake walivyochangia katika jamii. Wamekuwa zaidi ya warembo; ni watu wenye ushawishi na dira,” amesema.
Amebainisha kuwa baada ya kuendesha mashindano hayo kwa muda mrefu, waliona ni wakati wa kuachia nafasi hiyo kwa kizazi kipya chenye mawazo na ubunifu mpya.“Nilijiuliza nimkabidhi nani jukumu hili. Tulihitaji changamoto mpya, watu wenye nguvu na maono mapya. Ndipo tukafikia uamuzi wa kukabidhi kwa Lamata Village,” ameongeza.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Lamata Village, Grace Mgaya, amesema wanapokea jukumu hilo kwa uzito mkubwa na kuahidi kuleta mageuzi chanya katika mashindano hayo. “Tunapokea jukumu hili kwa mikono miwili na kwa uzito wake. Tunaahidi kulisimamia kwa weledi mkubwa,” amesema. SOMA: Amina Jigge aipeperusha Bendera ya Tanzania Miss Earth 2025
Ameongeza kuwa Lamata Village inalenga kurejesha hadhi ya Miss Tanzania na kuifanya kuwa jukwaa la kukuza vipaji na maadili.“Lamata si waandaaji wa shindano pekee, bali ni taasisi yenye dira ya kumjenga mtu,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi wa Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Abel Ndaga, amesema mashindano ya Miss Tanzania si urembo pekee bali ni jukwaa la kuibua viongozi wa baadaye.“Miss Tanzania si urembo tu, ni jukwaa linalozalisha viongozi na watu wenye mchango mkubwa katika taifa,” amesema.