Dar es Salaam. Jaji Mkuu Mstaafu, Profesa Ibrahim Juma na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir, wamesema kuundwa kwa Tume ya Kuchunguza matukio ya kabla na baada ya Oktoba 29 kumeipa Tanzania heshima kubwa kimataifa.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Juma alisema tume hiyo inaonesha uwezo wa nchi kushughulikia changamoto zake kwa uwazi na weledi.

“Kuwa na tume hii kunaonesha kwamba tuna uwezo mkubwa wa kushughulikia masuala makubwa kama hayo, tuna taasisi imara na tunafanya kazi kwa uwazi,” alisema.

Aliongeza kuwa matarajio ya kimataifa ni makubwa, hivyo ripoti ya tume hiyo inapaswa kuendana na viwango hivyo.

“Tunaiambia dunia kuwa tuna uwezo wa kutatua changamoto zetu wenyewe na kuzitafutia ufumbuzi,” alisisitiza.

Wajumbe wenye weledi wa kimataifa

Akizungumzia sifa ya tume hiyo, Profesa Juma alisema imeundwa na wataalamu wabobezi katika fani mbalimbali, akimtaja Mwenyekiti wake, Othman Chande, kuwa na uzoefu mkubwa wa kimataifa.

Alibainisha kuwa Jaji Chande amewahi kuongoza uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dag Hammarskjöld, pamoja na matukio ya Sudan katika jimbo la El Fasher.

Aidha, alisema mwenyekiti huyo aliwaelekeza wajumbe kuhakikisha ripoti yao inazingatia viwango vya kimataifa badala ya kutegemea sheria za ndani pekee.

Ukusanyaji wa ushahidi wa kina

Profesa Juma alitaja pia uhuru wa tume katika ukusanyaji wa ushahidi, akisema imetembelea maeneo yote yaliyoathiriwa na matukio hayo na kuzungumza na majeruhi, wafiwa na wananchi waliopoteza ndugu zao.

Mufti aonesha imani na Tume

Kwa upande wake, Dk Zubeir alisema ana matarajio makubwa na tume hiyo kutokana na weledi wa wajumbe wake na namna ilivyotekeleza majukumu yake hadi sasa.

“Naona tume ina umahiri mkubwa. Nina imani itafanya kazi nzuri na kutuweka katika nafasi nzuri,” alisema.

Alibainisha kuwa ameshiriki kutoa maoni yake mbele ya tume na kujiridhisha kuhusu uwezo wake.

Aidha, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda tume hiyo, akisema ni uamuzi wa busara unaolenga kutafuta ukweli na haki.

Tume yaongezewa muda

Wakati huohuo, tume hiyo imeongezewa muda hadi Aprili 24 mwaka huu ili kukamilisha kazi yake kwa ufanisi.

Hatua hiyo imelenga kukamilisha uchambuzi wa ushahidi pamoja na kutoa nafasi kwa wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi kuchambua vielelezo vipya.

Jumuiya ya kimataifa ikiwemo Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola zimeisifu Tanzania kwa kuunda tume hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *