Usalama wa baharini katika Mlango Bahari wa Hormuz ndio mada ya mkutano wa kimataifa leo Ijumaa hii, Aprili 17, jijini Paris. Mpango huu wa Ufaransa na Uingereza umeungwa mkono na nchi zaidi ya thelathini. Kwa kuwa meli kupita kwa sasa kwa mlango huo kumezuiwa na Iran na kizuizi kilichowekwa na Marekani kwenye bandari za Iran, lengo ni kujiandaa kwa mustakabali na kurejesha imani muhimu kwa meli za kibiashara katika eneo hili la dunia mara tu uhasama utakapokoma.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Hakuna swali la kukubali uwepo wa mabomu yanayotishia meli katika Mlango Bahari wa Hormuz. Hakuna swali la kuvumilia ushuru katika ukanda huu wa baharini ambao ni muhimu kwa uchumi wa dunia. Na hakuna swali la kubadilisha sheria za urambazaji katika mlango bahari huu, kama ilivyo katika bahari zote ambapo sheria za kimataifa zinapaswa kutumik. Kulingana na ofisi ya rais wa Ufaransa, mpango wa urambazaji katika Mlango Bahari wa Hormuz utategemea kanuni hizi tatu.

Nchi zaidi ya thelathini zinawakilishwa katika mkutano huu wa Aprili 17 jijini Paris, lakini orodha ya mwisho bado haijulikani. Miongoni mwa viongozi waliohusika ni Keir Starmer wa Uingereza, Friedrich Merz wa Ujerumani, na Giorgia Meloni wa Italia. Huko Paris, inadaiwa kwamba baadhi ya nchi zinazoshiriki zitaweza kutoa sauti zao kusikika na Marekani na Israel, huku zingine zikisikika na Iran.

“Sio operesheni ya kijeshi”

“Hii si operesheni ya kijeshi,” chanzo cha Ufaransa kinabainisha, “bali ni kupanga operesheni ya usalama itakayofanyika dhidi ya msingi wa usitishaji mapigano ulioimarishwa.” Changamoto inasalia kufikia makubaliano: Kansela wa Ujerumani Merz anabaini kwamba Marekani inaweza kujiunga na mpango huu. Hata hivyo, upande wa Ufaransa wanabainisha kwamba haiwezekani kuzijumuisha nchi hasimu.

Tangu kuzuka kwa vita nchini Iran na mahambulizi makali Mashariki ya Kati mnamo Februari 28, kuzuiwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, ambapo 20% ya mafuta na gesi duniani hupita, kumesababisha kuongezeka kwa bei za nishati ambazo zina uzito mkubwa kwa uchumi wa dunia. Ingawa usitishaji mapigano wa wiki mbili ulianza kutekelezwa Aprili 8, hali bado ni dhaifu baada ya kushindwa kwa mazungumzo ya Iran na Marekani, siku ya Jumapili ambayo yalilenga kuimarisha mpango huo.

Kujitolea kulingana na “uwezo”

Kila nchi inayoomba misheni hiyo itajitolea “kulingana na uwezo wake.” Ufaransa, kwa upande wake, ina meli ya kubeba ndege, takriban meli kumi, na ndege hamsini katika eneo hilo, Ikulu ya Élysée imebainisha. Berlin, kwa upande wake, inaweza kuchangia “kutegua mabomu au upelelezi wa baharini wa masafa marefu,” kulingana na chanzo cha serikali ya Ujerumani kilichonukuliwa na shirika la habari la AFP. Mkutano wa Ijumaa utafuatiwa wiki ijayo na “mkutano wa kimataifa” katika makao makuu ya pamoja ya kudumu huko Northwood, kaskazini magharibi mwa London, pia ukizingatia suala la Mlango-Bahari wa Hormuz, Downing Street imetangaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *