Kiungo wa Benfica, Gianluca Prestianni, ameadhibiwa kwa kufungiwa mechi sita baada ya kubainika kutoa kauli ya kibaguzi kwa Vinícius Júnior wakati wa mchezo dhidi ya Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi Februari.

Mchezo huo ulisimamishwa kwa dakika 10 baada ya Vinícius Júnior kumlalamikia mwamuzi François Letexier akidai ametukanwa kwa kauli ya kibaguzi akisema aliitwa nyani. Madai hayo yaliungwa mkono na mshambuliaji mwenzake, Kylian Mbappé.

Hata hivyo, uchunguzi wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) limebaini kuwa kauli iliyotolewa haikuwa ya ubaguzi wa rangi, bali ilikuwa ya ubaguzi wa kijinsia.

Prestianni amefungiwa mechi sita na adhabu hiyo itatumika katika mashindano ya Ulaya au akiwa na timu ya taifa ya Argentina. Adhabu hiyo pia inajumuisha kufungiwa kwa muda alikokuwa ametumikia awali.

Winga wa Real Madrid, Vinicius Jr akiwa katika mgogoro na nyota wa Benfica, Gianluca Prestianni wakati akidai kutolewa maneno ya kibaguzi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Februari 17, 2026. Picha na Mtandao

Utetezi wa mchezaji

Prestianni amekanusha vikali tuhuma hizo, akisisitiza kuwa hajawahi kuwa mbaguzi.

“Nimeumizwa sana kuitwa mbaguzi wa rangi kwa jambo ambalo sikulifanya. Niliadhibiwa bila ushahidi,” amesema katika mahojiano.

Awali, kiungo wa Real Madrid, Aurélien Tchouaméni, alidai kuwa mchezaji huyo alikiri kutoa kauli ya ubaguzi wa kijinsia badala ya ule wa rangi.

Kocha wa Benfica, Jose Mourinho. Picha na Mtandao

Kauli ya Mourinho

Kocha wa Benfica, José Mourinho, amesema iwapo itathibitika kuwa mchezaji wake alitoa kauli ya ubaguzi wa rangi, basi hatakuwa na nafasi tena klabuni hapo.

Hata hivyo, hakufafanua hatua atakazochukua iwapo tuhuma za ubaguzi wa kijinsia ndizo zitathibitishwa.

Tukio hilo linaongeza mjadala mpana kuhusu nidhamu na vitendo vya ubaguzi katika soka la Ulaya, huku mamlaka zikisisitiza kutovumilia aina yoyote ya lugha ya chuki uwanjani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *