
Kishapu. Katika hatua ya kukabiliana na mikopo yenye riba kubwa maarufu kama kausha damu, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu limeazimia kufanya uchunguzi katika taasisi za mikopo midogo (microfinance) ili kubaini uhalali wa riba zinazotozwa.
Azimio hilo limetolewa Aprili 24, 2026 wakati wa kikao cha baraza hilo, ambapo madiwani walisisitiza umuhimu wa kulinda wananchi dhidi ya mikopo yenye masharti magumu yasiyozingatia sheria za fedha.
Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa Viti Maalumu kata ya Sekebugoro, Ajihath Kasenene amesema Halmashauri ina wajibu wa kufuatilia kwa karibu taasisi za huduma ndogo za kifedha ili kuhakikisha riba wanazotoza ni halali na rafiki kwa wananchi.
Amesema baadhi ya taasisi zimekuwa zikitoza riba kubwa inayowaumiza wakopaji na kuwafanya kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati, hali inayochangia kuongezeka kwa malalamiko miongoni mwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo, baraza hilo limependekeza kufanyika kwa uchunguzi wa kina utakaosaidia kubaini taasisi zinazokiuka taratibu na kuchukua hatua stahiki za kisheria.
“Ili kuhakikisha sheria ya kifedha zinafuatwa Halmashauri inatakiwa kufutilia na kuchunguza riba za taasisi ndogo za mikopo, hasa ya kausha damu na kuhakikisha riba zake ni rafiki kwa wananchi, sio kuwatesa kiuchumi” amesema Ajihath.
Kutokana na hoja hiyo, baraza hilo lililoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Josephat Limbe, limeazimia kufanyika kwa uchunguzi wa kina na ufuatiliaji wa riba zinazotozwa na taasisi ndogo za mikopo, kwa lengo la kulinda maslahi ya wananchi na kuhakikisha zinazingatia sheria za kifedha.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo, Fabiani Makongo amepongeza juhudi za madiwani kwa kusimama kidete kutetea maslahi ya wananchi, hususan wajasiriamali wadogo.
Amesema hatua hiyo inaleta matumaini mapya na kuimarisha imani ya wananchi kwa viongozi wao.
“Msimamo huu wa madiwani unachochea hali ya wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya eneo lao, huku akibainisha kuwa ulinzi wa masilahi ya wajasiriamali ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa ndani,” amesema Makongo.
Ofisa usafirishaji wilayani humo, Ezra Leonard amesisitiza kuwa uongozi unaojali na kusikiliza wananchi ni chachu ya maendeleo endelevu, na kwamba juhudi hizo zinapaswa kuendelezwa ili kujenga jamii yenye ustawi, mshikamano na fursa sawa kwa wote.