Kibaha. Katika kuhakikisha huduma katika Hopsitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani  Tumbi zinaboreshwa Kampuni ya GFA  imetoa msaada wa vifaatiba na vitendea kazi hospitalini hapo.

Hatua hiyo  inayolenga kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta nne, vifaa vya kuhifadhia taka, ambavyo vinatarajiwa kuongeza ufanisi katika shughuli za kila siku hospitalini hapo.

Akizungumza jana Aprili 24, 2026 baada ya kupokea msaada huo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Silas Msangi, alisema hatua hiyo ina mchango mkubwa katika kuimarisha huduma za afya.

“Tunashukuru kwa msaada huu wa vitendea kazi. Hii ni ishara ya ushirikiano mzuri kati ya sekta binafsi na Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya,” alisema Dk Msangi.

Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda cha GFA, Ezra Merei, alisema kampuni hiyo imeamua kuadhimisha miaka yake 19 kwa kurejesha sehemu ya mafanikio yake kwa jamii.

Alieleza kuwa pamoja na shughuli kuu ya kampuni hiyo kuwa ni uunganishaji wa magari, bado wanaamini kuwa ustawi wa jamii unaowazunguka ni msingi wa maendeleo yao.

“Afya ni muhimili wa uchumi. Bila watu kuwa na afya njema, uzalishaji hauwezi kufanyika. Ndiyo maana tuna utaratibu wa kurejesha kwa jamii kupitia programu zetu za uwajibikaji kwa jamii (CSR),” alisema Merei.

Akizungumza hospitalini hapo mmoja wa wagonjwa aliyeshuhudia makabidhiani hayo, Mwajuma Mbonde alisema kuwa anaamini kila mwekezaji anaoaswa kuisaidia jamii inayozunguka mradi, akiipongeza kampuni hiyo kwa kuboresha mazingira ya wagonjwa kupata huduma ya matibabu.

“Kampuni zote zilizowekeza nchini zingefanya kama hawa, naamini maeneo mengi yangekuwa bora katika utoaji huduma, badala ya kuiachia Serikali peke yake,”alisema Mwajuma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *